Katika adabu na hukumu za kuutembelea Msikiti wa bwana Mtume:
Katika adabu na hukumu za kuutembelea Msikiti wa bwana Mtume:
These files are generated automatically from the book's text; their layout may differ from the printed edition.
Katika adabu na hukumu za kuutembelea Msikiti wa bwana Mtume:
Ameipokea hadithi hii Imamu Bukhari (1189) na Imamu Muslimu (827) na tamko la hadhithi hii ni la Muslimu.
Ameipokea Imamu Bukhari (1190) na Imamu Muslimu (1394).
Ameipokea Imamu Bukhari (1195) na Muslimu (1390).
Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote, na rehema na amani ziwe juu ya Mtume wetu Muhammad, na watu wake na Maswahaba zake wote.
Ama baada ya hayo:
Ujumbe huu mfupi unahusu adabu na hukumu za kuutembelea Msikiti wa bwana Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Tumepupia ndani ya ujumbe huu, kuweka wazi mambo ambayo kwa kawaida anayahitajia mwenye kuutembelea Msikiti wa bwana Mtume.
Na tunamuomba Mwenyezi Mungu aufanye uwe kwa ajili ya uso wake Mtukufu, na kwamba awanufaishe kwa ujumbe huu Waislamu wote.
Kamati ya Kisayansi ya Jumuia ya Huduma ya Maudhui za Kiislamu kwa Lugha mbalimbali.
Muhtasari:
Inapendekezwa kuutembelea Msikiti wa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na hakuna wakati maalumu wa kuutembelea na wala hilo siyo miongoni mwa matendo ya Hija, na wala siyo lazima mahujaji - wa kiume au wa kike - kutembelea kaburi la Mtume, rehema na mani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, wala siyo lazima kutembelea Baqiiy (Makaburi ya Madina).
Hairuhusiwi kufunga safari ndefu kwa ajili tu ya kutembelea kaburi la Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Kwa maana kufunga safari kwa malengo ya kiibada hakuwi kwa ajili ya kuyatembelea makaburi. Bali hilo linakuwa kwa ajili ya kuitembelea ile misikiti mitatu tu. Amesema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Isifungwe safari ndefu isipokuwa kwenda kwenye misikiti mitatu: Msikiti wangu huu, Msikiti wa Makkah na Msikiti wa Aqswaa (uliopo Palestina)."
Basi kwa yule aliye mbali na mji wa Madina hafai kufunga safari ndefu kwa malengo ya kutembelea kaburi la Mtume, lakini ameruhusiwa kisheria kufunga safari ndefu kwa malengo ya kutembelea Msikiti mtukufu wa Mtume. Akifika katika msikiti huo, atatembelea kaburi lake Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na pia atatembelea makaburi ya Maswahaba zake. Kwa hivyo kutembelea kaburi lake Mtume kukawa kumeingia katika kuutembelea msikiti wake - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.
Haifai kisheria kwa mwanamke kutembelea kaburi la Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, wala kutembelea kaburi la yeyote asiyekuwa Mtume, kwa sababu yeye Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, aliwalaani wanawake wenye kutembelea makaburi, kwa kuhofia huenda wakaomboleza kwa njia iliyokatazwa, na kutoka bila kujisitiri, na makosa mengineyo ya kisheria. Hata hivyo, ni sunna kwao kukithirisha kumtakia rehema na amani Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, nalo ni jambo linaweza kufanyikia mahala popote ambapo mwanamke atakuwa; kwa mujibu wa kauli yake, rehema na amani ziwe juu yake: "Msizifanye nyumba zenu kuwa makaburi, na wala msilifanye kaburi langu kuwa sikukuu (yaani mahali pa kwenda mara kwa mara), na mniombee rehema, kwani maombi yenu hunifikia mahala popote mtakapokuwa." Na amesema Mtume, rehma na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: “Hakika Mwenyezi Mungu ana Malaika wanaozunguka katika ardhi wanaonifikishia salamu kutoka kwa umma wangu."
Atakapoingia katika msikiti mtakatifu wa Mtume, inapendekezwa kwamba autangulize mguu wake wa kulia wakati wa kuingia na aseme: "Allahummaf tah-liy ab-waaba rahmatika." Yaani: "Ewe Mwenyezi Mungu, nifungulie milango ya rehema zako." Kama atakavyosema maneno hayo wakati atakapoingia misikiti mingine.
Na hakuna dhikri maalumu wakati wa kuingia kwenye Msikiti wa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake.
Kisha ataswali rakaa mbili za Tahiyyatul masjid (maamkizi ya msikiti).
Na ikiwa wakati huo alioingia msikitini, siyo wakati ambao umekatazwa kuswali sunna, basi anaweza kuswali swala za sunna rakaa mbilimbili kwa namna atakavyotaka. Amesema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Swala moja iswaliwayo kwenye Msikiti wangu huu ni bora kuliko swala elfu moja zinazoswaliwa kwenye misikiti mingine, isipokuwa swala iswaliwayo kwenye Msikiti Mtakatifu wa Makkah."
Na inapasa kupupia na kujitahidi kuswalia katika Raudhwa (nayo ni sehemu iliyopo kati ya Mimbari na chumba cha Mtume, rehema na amani ziwe juu yake) ikiwa ni rahisi kwake kuswalia mahala hapo; kwa kauli yake Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Sehemu iliyopo kati ya mimbari yangu na nyumba yangu ni bustani miongoni mwa bustani za Peponi."
Na ikiwa haitokuwa rahisi kwake kuswalia katika Raudhwa, basi ataswalia upande wowote wa msikiti. Na kuswalia huko siyo katika swala za jamaa. Kwani kama swala ni ya jamaa, basi na adumu kuiswalia katika safu ya kwanza nyuma ya imamu; kwa ujumla wa ushahidi uliopokelewa kuhusu jambo hilo.
Na akitaka kutembelea kaburi la Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, na makaburi mawili ya Maswahaba zake wawili (Abubakari na Omari):
Atasimama kwa heshima na utulivu mbele ya kaburi lake Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na atapunguza sauti, kisha atamsalimia Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na atasema hivi: "Assalam alaika ya rasuulallah warahmatullahi wabarakaatuhu (Amani iwe juu yako ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, na rehema zake na baraka zake)." Na ikiwa tasema: "Ash-hadu annaka rasuulullah haqqan, wa-annaka qad ballaghtar-risalata, wa addaital amaanata, wa jaahadta fillahi haqqa jihaadihi, wanaswahtal umma, fajaazakallahu 'an ummatika afdhwala ma jazaa nabiyyan 'an ummatihi (Ninashuhudia kweli kuwa wewe ni Mtume wa haki wa Mwenyezi Mungu, na kwamba uliufikisha ujumbe, na ukatekeleza amana, na ukapigana jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu haki ya kumpigania, na ukaupa umma nasaha. Basi Mwenyezi Mungu akulipe malipo yaliyo bora zaidi kwa namna alivyomlipa Nabii kwa ajili ya kuuhudumia umati wake)." basi hakuna ubaya katika hilo.
Kisha atasongea kidogo upande wa kulia, na atamsalimu Abuubakari Swiddiq - radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.
Kisha atasongea vilevile upande wa kulia kidogo na atamsalimu Omari bin Khattwab. Alikuwa bin Omari, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na baba yake, anapomsalimia Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na hao Maswahaba zake wawili - kwa kawaida hakuwa akizidisha zaidi ya kusema: "Assalamu 'alaika yaa rasuulallahi. Assalamu 'alaika yaa Abaabakri. Assalamu 'alaika ya abataah (Amani iwe juu yako ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Amani iwe juu yako ewe Abuubakari. Amani iwe juu yako ewe baba yangu)." kisha anaondoka.
Na wala haipasi kurefusha kisimamo au kurefusha dua mbela ya kaburi la Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - wala mbele ya mskaburi ya hao Maswahaba zake wawili. Jambo hilo limechukiwa na Imamu Maalik, na akasema: "Jambo hilo ni uzushi ambao hawakulifanya wema waliotangulia. Na hautokuwa mwema umma huu wa mwisho isipokuwa kwa kile kilichowafanya wawe wema waliotangulia."
Na ama mambo wanayoyafanya baadhi ya wenye kufanya ziara kama vile kuinua sauti juu mbele ya kaburi la Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - na kusimama hapo kwa mda mrefu, jambo hilo ni kinyume na sheria; kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Enyi mlioamini! Msinyanyue sauti zenu kuliko sauti ya Nabii, wala msiseme naye kwa kelele kama mnavyosemezana nyinyi kwa nyinyi, visije vitendo vyenu vikaharibika, na hali hamtambui. Kwa hakika wale wanaoteremsha sauti zao mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, hao ndio Mwenyezi Mungu amezisafisha nyoyo zao kwa uchamungu. Hao watakuwa na maghfira na malipo makubwa." [Al-Hujurat: 2- 3] Na kwa sababu kusimama kwa muda mrefu kaburini kwake, rehema na amani ziwe juu yake, na kumtolea salamu kwa wingi kunasababisha msongamano, kelele nyingi, na sauti kubwa kwenye kaburi lake, rehema na amani ziwe juu yake, na hilo linakwenda kinyume na yale ambayo Mwenyezi Mungu amewawekea sheria Waislamu katika Aya hizi zenye maana za wazi. Na Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, anaheshimika akiwa hai na maiti. Kwa hivyo, Muumini hafai kufanya mambo yanayokwenda kinyume na adabu za Kiislamu kwenye kaburi lake.
Na vile vile wanayoyafanya baadhi ya wenye kutembelea makaburi haya na wengineo ya kupupia kuombea dua kwenye kaburi lake akiwa ameelekea kaburi hali ya kuinua mikono yake huku akiomba. Haya yote ni kinyume na walivyokuwa wakifanya wema waliotangulia miongoni mwa Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na wafuasi wao waliowafuata kwa wema. Bali kufanya hivyo ni katika uzushi uliozushwa.
Na vile vile wanayoyafanya baadhi ya wenye kufanya ziara wakati wanapomsalimia Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ya kuweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto juu ya kifua chake au chini ya yake, kama anavyofanya mtu anayeswali. Namna hii haifai wakati wa kumsalimia Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake; kwa sababu ni namna ya kujidhalilisha, kunyenyekea na ni ibada ambayo hafai kufanyiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake, kama alivyoelezea Al-Haafidhi bin Hajar kutoka kwa maulamaa katika kitabu kiitwacho "Al-Tat-hu".
Na wala haruhusiwi yeyote kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kujipangusa kwenye chumba cha Mtume au kukizunguka, na wala asimuombe Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, amtekelezee haja zake, au amponyeshe ugonjwa wake, na mfano wa hayo. Kwa sababu, hayo yote haombwi isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake.
Inapendekezwa kwa mwenye kuutembelea mji wa Madina, wakati wa kuwepo kwake katika mji huo autembelee msikiti wa Qubaa na aswali humo; kwa sababu Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alikuwa akiuendea msikiti huo wa Qubaa kwa kutumia kipando na wakati mwingine kwa kutembea kwa miguu na kuswali humo rakaa mbili. Imepokelewa hadithi kutoka kwa Sahal bin Haniif kwamba amesema: Amesema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Mwenye kujitwaharisha nyumbani kwake, kisha akaenda katika msikiti wa Quba na akaswali humo swala moja, anapata malipo sawa na aliyefanya ibada ya Umra."
Na ni Sunna kwa wanaume kuzuru makaburi ya Al-Baqi’i, makaburi ya wale waliouawa kwa ajili ya dini (mashahidi) na kaburi la Hamza, Mwenyezi Mungu amuwie radhi. Kwa sababu Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alikuwa akiwatembelea na kuwaombea dua, na kwa sababu alisema: "Nilikuwa nimekukatazeni kutembelea makaburi. Basi sasa yatembeleeni, kwani hakika kutembelea makaburi kunakukumbusheni akhera."
Na atasema atakapowatembelea kama anavyosema anapoyatembelea makaburi mengine: "Assalamu 'aalikum ahlad-diyaari minal muuminiina walmuslimiina, wa innaa in shaa Allahu bikum laahiquun. Wayarhamullahul mustaqdimiina minna walmusta-aakhiriina. Nas-alullaha lanaa walakumul aafiyat (Amani ya Mwenyezi Mungu iwe nanyi, enyi wakazi wa makazi haya, miongoni mwa Waumini na Waislamu, na sisi hakika akitaka Mwenyezi Mungu tutaungana nanyi. Awahurumie Mwenyezi Mungu waliotangulia miongoni mwetu na waliochelewa. Na tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe salama sisi pamoja nanyi)."
Na hapana shaka kuwa makusudio ya kutembelea makaburi ni kukumbuka Akhera na kuwafanyia uzuri maiti kwa kuwaombea dua, na kufuata sunna ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Hii ndiyo ziara ya kisheria.
Na ama kuwatembelea kwa lengo la kuombea kwenye makaburi, au kumuomba Mwenyezi Mungu kupitia wao au utukufu wao, na mfano wa hayo, ziara ya aina hii ni uzushi na ni uovu hakuiwekea sheria hiyo Mwenyezi Mungu wala Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na wala hawakufanya hivyo wema waliotangulia. Ama kuwaomba wao kukidhi haja mbalimbali, au kuwaponyesha wagonjwa, na mfano wake, hayo ni katika ushirikina mkubwa.
Na ninakuletea ewe msomaji baadhi ya Hadithi hizi zilizotungwa na watu katika mlango huu; ili uzijue na ujihadhari na kudanganyika nazo:
Hadithi ya kwanza: 'Yeyote atakayefanya Hija kisha asinitembelee, kwa hakika mtu huyo kanitenga.'
Hadithi ya pili: 'Yeyote atakayenitembelea baada ya kufa kwangu, ni kama amenitembelea wakati wa uhai wangu.'
Hadithi ya tatu: 'Atakayenitembelea na akamtembelea baba yangu Ibrahim ndani ya mwaka mmoja, basi nimemdhaminia Pepo kwa Mwenyezi Mungu.'
Ya nne: 'Mwenye kutembelea kaburi langu, basi lazima atapata uombezi wangu.'
Hadithi hizi na mfano wake hakuna chochote kwazo kilichothibiti kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Amesema Al-Haafidh Al-'Uqailiy: "Haikupokelewa hadithi yoyote iliyo sahihi katika mlango huu." Na akasema Al-Hafidh bin Hajar katika kitabu kiitwacho At-Talkhiis - baada ya kutaja riwaya hizi nyingi - "Njia za upokezi wa hadithi hizi zote ni dhaifu." Si katika Sunna za Hija na Umra au ukamilifu wa Hija na Umra kuutembelea Msikiti wa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kabla au baada ya Hija na Umra, kwa sababu kuutembelea Msikiti wa Mtume ni sunna na wala si vinginevyo. Hivyo basi, ikiwa mwenye kufanya Hija au Umra hakuutembelea, hapati dhambi, na wala hakuna mafungamano kati Hija na Umra na kutembelea Msikiti wa Mtume, kwani, hizo ni ibada mbili tofauti. Basi mtu yeyote atakayefanya Hija au Umra, si lazima kwake kuutembelea Msikiti wa Mtume. Vilevile, mwenye kuutembelea Msikiti wa Mtume si lazima kwake kufanya Hija au Umra, na ikiwa atakusanya Hija na Umra na kuutembelea Msikiti wa Mtume katika safari moja, basi hakuna ubaya.
Makosa yafanyikayo katika kuutembelea msikiti wa Mtume:
1. Kujipangusa kwenye kuta na nguzo za chuma wakati wa kutembelea kaburi la Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na kufunga nyuzi na mfano wake kwenye madirisha kwa ajili ya kutafuta baraka.
Hayo yote si sahihi. Kwani baraka hupatikana katika jambo ambalo ameliweka Mwenyezi Mungu na Mtume wake na siyo katika jambo la uzushi.
2. Kwenda kwenye mapango yaliyopo kwenye mlima Uhudi na mfano wake kama vile pango la Hiraa na Thauru katika mji wa Makkah na kufunga matambara mlimani hapo, na kuomba dua ambazo hakuziidhinisha Mwenyezi Mungu na ni kujibebesha ugumu katika kufanya mambo hayo.
Mambo yote haya ni uzushi usiokuwa na asili katika sheria tukufu.
3. Kutembelea baadhi ya sehemu ambazo wanadai kuwa sehemu hizo zina athari za Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kama vile sehemu alipopiga magoti ngamia na kisima cha pete au kisima cha Othman, na kuchukuwa udongo kutoka katika maeneo haya kwa ajili ya kutaka baraka.
4. Kuwaomba maiti wakati wa kutembelea makaburi ya Baqii, na makaburi ya wale waliouawa kwa ajili ya dini (mashahidi wa) pale Uhudi, na kutupa pesa kwenye makaburi hayo kwa ajili ya kujikurubisha kwa maiti hao, na kutaka baraka kwa waliozikwa humo.
Haya ni katika makosa makubwa, bali ni katika ushirikina mkubwa kama walivyoyataja maulamaa, na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunnah za Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, vikayaashiria makosa hayo. Kwa sababu, ibada ni ya Mwenyezi Mungu peke yake na wala haifai kufanya chochote katika ibada hizo na kukielekeza kwa mwingine, kama vile dua, kuchinja, kutia nadhiri na mfano wa hayo. Haya ni kwa mujibu wa maneno yake Mwenyezi Mungu: "Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini." [Al-Bayyinah :5]
Na Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi, na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Mtume wetu Muhammad, na juu ya watu wake na Maswahaba zake wote.
Related books
All books
Kuutembelea Msikiti Ntukufu Wa Mtume Na Baadhi Ya Tanbihi Na Muongozo Kwa Mwenye Kuutembelea14 lughaKuutembelea Msikiti Ntukufu Wa Mtume Na Baadhi Ya Tanbihi Na Muongozo Kwa Mwenye Kuutembelea
Mtunzi: Dr. Abdallah Bin Najiy Al Mikhlafy Kwa Jina La Mwenyezi Mungu Mwingi Wa Rehma Mwenye Kurehemu Utangulizi Kila sifa kamilifu zinamstahiki Allah ambae amejaalia msikiti wa Mtume Mtukufu- Rehma na amani ziwe juu yake- ni katika ibada kubwa,na akajaalia kuswali ndani yake ni uongeza darja, nwala na amani ziwe juu ya Mtume wetu Muhammad ambae ni kiumbe mtakatifu, na ziwe juu ya familia yake na maswahaba zake na wote walio wafuata Maswahaba kwa wema mpaka siku ya kifo.
Fadhila na adabu za Msikiti wa bwana Mtume na hukumu za kuzuru kaburi la Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na kaburi za Maswahaba zake wawili, Mwenyezi Mungu awe radhi nao52 lughaFadhila na adabu za Msikiti wa bwana Mtume na hukumu za kuzuru kaburi la Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na kaburi za Maswahaba zake wawili, Mwenyezi Mungu awe radhi nao
Kitabu kinabainisha fadhila za Msikiti wa Mtume na adabu za kuutembelea, vile vile kinaeleza adabu za kulizuru kaburi la Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na makaburi ya maswahaba zake wawili, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, huku kikisisitiza umuhimu wa utulivu na usafi na kujiepusha na matendo ya uzushi wakati wa ziara.
(Kitabu cha Adabu za kwenda katika Swala)11 lugha(Kitabu cha Adabu za kwenda katika Swala)
Mtunzi: Sheikh Al- islaam na alama miongoni mwa alama, kiongozi aliyerudisha upya elimu ya dini, Sheikh Muhammad bin Abdulwahhab Allah Mtukufu amrehemu. Wamefanya kazi ya kusahihisha na kulinganisha Nakala iliyoandikwa kwa mkono katika Maktaba ya Saudia kwa namba 269/86 na nakala nyingine nyingi zimechapishwa na masheikh wafuatao: Abdul karim bin Muhammad Al-laahim. Naasir bin Abdillahi Al- Twariim, Suud bin Muhammad Al- bashar. Kwa Jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu: (Mlango wa adabu za kwenda katika Swala) Ni Sunna kutoka kuiendea swala hali ya kuwa umejitwaharisha…
MUHTASARI WA NAMNA YA KUFANYA UMRAH NA HUKUMU ZAKE65 lughaMUHTASARI WA NAMNA YA KUFANYA UMRAH NA HUKUMU ZAKE
Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote, na rehema na amani ziwe juu ya Mtume wetu Muhammad, na watu wake na Maswahaba zake wote. Ama baada ya hayo: Hii ni makala fupi juu ya namna ya kufanya Umra, hukumu zake na adabu zake. Tumejitahidi kubainisha ndani yake mengi katika yale anayohitaji mtu anayefanya ‘Umra. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aifanye iwe kwa ajili ya uso wake mtukufu, na kwamba anufaishe kwayo Waislamu wote.