Kumfundisha Muislamu Mpya
Kitabu cha kumfundisha Muislamu mpya kinatoa mtaala mwepesi wa kufundisha mambo ya msingi ya Uislamu kwa Muislamu anayeanza, hivyo kinafafanua itikadi na nguzo za Uislamu na imani, na kinabainisha hukumu za twahara na swala, na kinaonyesha Maisha ya Mtume, rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani, na tabia (Maadili) na ibada kwa njia nyepesi. Vilevile kinaimarisha Tawhidi (kumpwekesha Mwenyezi Mungu), na kinasaidia katika kujenga uhusiano ulio sahihi na Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuishi kulingana na mfumo wa Uislamu.
This PDF is generated automatically from the book's text; its layout may differ from the printed edition.
Kumfundisha Muislamu Mpya
Mtunzi
Jumuiya inayoitwa Waqt Al-hiwaar
Somo la Kwanza:
Inamaanisha nini kuingia katika Uislamu?
Ndugu yangu Muislamu; pokea bishara njema ya siku bora inayokupitia.. na wakati wenye furaha zaidi ambao upo ndani yake.. pale ulipotangaza kusilimu kwako kwa Mwenyezi Mungu!
Kwanza kabisa.. tunapenda kukupongeza kwa uamuzi huu mkubwa, ambao unahesabika kuwa ni uamuzi muhimu zaidi katika maisha yako; kwani hakika neema kubwa zaidi ya Mwenyezi Mungu kwako ni kukuongoza na kukuwezesha kuingia katika Uislamu ambao ameuridhia kwa waja wake kuwa ndiyo dini, na tunakupa habari njema kwamba Mwenyezi Mungu anabadilisha maovu yako kuwa mema.. na anakusamehe madhambi yako yaliyotangulia, kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur-ani kuhusu hali ya yule aliyetubia: "Isipokuwa atakayetubu, na akaamini, na akatenda matendo mema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kurehemu." [Al Furqaan: 70].
Ndugu Muislamu; ukitazama kando yako, utaona watu wengi hawakuwezeshwa kama wewe kufikia dini ya haki, na kuwezeshwa huku ni fadhila za Mwenyezi Mungu anazompa yule ambaye ameona ndani ya moyo wake kutamani kuipata haki, sio kwa juhudi yako, bali hakika kwanza ni kuwezeshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwako.
Na jua kwamba neema hii hailingani na neema nyingine, basi vyovyote utakavyokajukumishwa na kuvumilia kwa ajili ya kuihifadhi, ni jambo jepesi. Kwani Mwenyezi Mungu amewaumba waja, Naye amejitosheleza na hawahitaji, na haki yake juu yao ni wamuabudu, na wasimshirikishe na chochote. Naye hana haja ya ibada yao, bali wao ndio wanaohitaji kumuabudu na uongofu wake; kwa sababu ndani yake mna furaha yao katika dunia na Akhera.
Kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Basi yule ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumuongoa, humfungulia kifua chake kwa Uislamu..." [Al-An'am: 125].
Somo la Pili:
Lengo la Maisha
Wengi miongoni mwa wanafikra na watu wa kawaida sawia wanatatizika katika majibu ya swali muhimu zaidi katika maisha yetu:
Kwa nini sisi tupo? Au: Ni lipi lengo la maisha yetu?
Qur'ani imebainisha lengo la kuwepo mwanadamu katika maisha haya kwa uwazi na usahihi kabisa, katika maneno ya Mwenyezi Mungu: "Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi." [Surat Adh-Dhariyaat: 56], Hivyo kumuabudu Muumbaji ndiyo lengo la kuwepo kwetu katika ardhi hii, na vyote vinginevyo ni nyenzo, vifuatizi na vikamilishi.
Lakini Ibada katika Uislamu si utawa na kujitenga kabisa na maisha na starehe zake, bali inakusanya pamoja na ibada zilizofaradhishwa (kama vile: Sala, Funga na Zaka) matendo yote ya mwanadamu na kauli zake na tabia zake na mahusiano yake, bali hata michezo yake na starehe zake; pindi yanapoambatana hayo na nia njema na kusudio zuri, na kwa ajili hiyo alieleza Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kuwa kustarehe mume na mke wake wanapata kwayo malipo ikiwa ni kwa nia ya kujiweka mbali na haramu, au wazae kwayo kizazi chema.
Na kwa hilo anatambua Muislamu kuwa kila anachokifanya katika maisha yake miongoni mwa mambo ya dunia; kama vile kufanya juhudi katika kutafuta riziki, na ndoa, au anayoyafanya miongoni mwa ibada kama vile swala na sadaka, atapata kwayo thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na hakika Qur'ani imeashiria dhana hii katika sehemu nyingi.
Somo la Tatu:
Nani ndiye Mungu wa kweli?
Maana ya Al-Ilaahu:
Mungu: Ni kila kinachofanywa kuwa muabudiwa, na hakika miungu inayoabudiwa imekuwa mingi kupitia historia ya mwanadamu, na yote katika Uislamu ni miungu batili, isipokuwa Mungu mmoja, Yeye ndiye Mungu wa kweli.
Ni nani Mungu wa kweli?:
Mungu wa kweli: Yeye ndiye ambaye hoja, akili iliyo sahihi na maumbile ya asili vimeonyesha kwamba Yeye peke yake ndiye anayestahiki kuabudiwa, na kwamba chochote kisichokuwa Yeye miongoni mwa miungu ni batili, hakistahili kuabudiwa.
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Hakuna mungu isipokuwa Yeye." Yaani: Hakuna muabudiwa kwa haki zaidi yake.
Yeye ndiye Allah (Mwenyezi Mungu), na Allah ndilo jina kuu la Mola wetu Mlezi, na halitumiwi kwa mwingine zaidi yake, na anao mkusanyiko wa majina mazuri yanayomhusu Yeye peke yake asiyekuwa yeye, naye ndiye mwenye kusifika na sifa za ukamilifu uliotimia, basi Yeye ndiye Mola wa kweli, yaani: Mola pekee anayestahiki kuabudiwa; kwa sababu Yeye peke yake ndiye muumba wetu, na mwenye kuturuzuku, na muendeshaji wa mambo yetu, na mwenye kujibu dua zetu, na ambaye mkononi mwake mna manufaa na madhara.
Ama kinachoabudiwa kinyume na Mwenyezi Mungu, basi hicho hakistahiki kuabudiwa; kwa sababu hakimiliki manufaa wala madhara, wala uhai wala kifo, wala uumbaji wala umiliki wala uendeshaji wa mambo.
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Hivi ni kwa sababu, Mwenyezi Mungu ndiye wa kweli, na hakika wanachokiomba ni cha uongo. Na kwamba hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mtukufu na ndiye Mkubwa." [Luqman: 30].
Basi mwanadamu akijua kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mungu wa kweli, inamlazimu kumwabudu Yeye pekee asiye na mshirika wake, na kumtii katika yale aliyoyaamrisha, na kuacha kuabudu visivyokuwa Yeye, na hii ndiyo maana ya kauli yetu: Laa ilaaha illa llaah, Yaani: Hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu.
Majina ya Mola wa haki:
Mwenyezi Mungu anajulikana kwa majina yake mazuri zaidi na sifa zake, nayo ni majina yanayojulisha ukamilifu wake na utukufu wake, na sifa zinazolingana na ukubwa wake.
Na miongoni mwa majina haya: Muumbaji, Mwingi wa rehema, Mwingi wa kurehemu, Mjuzi, Mwenye hekima, Mwenye kushinda.
Na miongoni mwa majina yake ni 'Al-Hayyu', aliyehai yaani: yule anayesifiwa kwa kuwepo kwa kudumu, uhai na kubakia milele, hivyo hafikiwi na kutoweka wala kumalizika.
Na 'Msimamizi', yaani: Anayejisimamia mwenyewe na anayesimamia kila kitu.
Na miongoni mwa majina yake pia ni 'Al-Haqq), kwa hivyo maneno yake ni ya kweli hayabadiliki, na ahadi yake ni ya uhakika, na matendo yake yote ni ya kweli na ya uadilifu na ya hekima, basi Yeye ni wa kweli kwenye dhati yake, na wa kweli katika sifa zake, na wa kweli katika matendo yake, na wa kweli katika amri yake na makatazo yake, na chochote kisichokuwa Yeye miongoni mwa vinavyoabudiwa ni batili.
Kumuamini Mungu wa kweli:
Kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mungu wa kweli aliye wazi ndiyo asili ya imani, na inalazimu kumpwekesha katika ibada peke yake asiye na mshirika.
Somo la Nne:
Jambo muhimu zaidi ninalowajibika nalo katika Uislamu (Nguzo za Uislamu)
Mwenyezi Mungu amewajibisha kwa kila Muislamu mwanamume na mwanamke mambo matano, ambayo ndiyo msingi wa Uislamu na nguzo zake, na yanaitwa 'Nguzo za Uislamu', nayo ni matendo ya dhahiri anayoyatekeleza Muislamu katika maisha yake, nayo ni:
1- Ni kushuhudia kuwa hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.
2- Kutekeleza Swala tano katika kila siku.
3- Kutoa Zaka mara moja kila mwaka kwa mafakiri na masikini na wengineo.
4- Kufunga mwezi wa Ramadhani.
5- Kuhiji Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu katika mji wa Makkah, kwa mwenye uwezo wa kwenda huko.
Nguzo za Uislamu na maelezo yake kwa ufupi:
1- Kushuhudia kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, na kuwa Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu:
Kushuhudia kuwa hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kuwa Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, ina maana: kuitakidi kwa yakini kuwa Mwenyezi Mungu ndiye muabudiwa wa kweli peke yake asiye na mshirika, na kuwa Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Na utamkaji wa shahada hii huwa ni kwa mtu kusema: "Ash-hadu an laa ilaaha illa llaah, wa ash-hadu anna Muhammadan rasuulullaah (Nashuhudia kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, na ninashuhudia kuwa Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu)", na hili ni tangazo la kwanza kutoka kwa mtu kuwa ameingia katika dini ya Mwenyezi Mungu, na amekuwa Muislamu, na ni wajibu kwake aanze kujifunza hukumu za dini yake, na kujua yale aliyowajibishiwa; ili Uislamu wake uwe sahihi, na zipatikane kwake radhi za Mola wake Mlezi, na kuingia Peponi.
❖ Maana ya kushuhudia kuwa "Hakuna mungu apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu":
Hakuna mungu apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu, na tamko hilo ndilo tunaloliita 'Tauhidi', na inamaanisha kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika ibada, hivyo usimshirikishe na yeyote asiyekuwa Yeye, katika kumuomba, au kuswali kwa ajili yake, au kufanya utiifu kwa ajili yake, bali uzifanye ibada zako zote akusudiwe kwazo Mwenyezi Mungu, ukitarajia thawabu kutoka kwake, na kuogopa adhabu kutoka kwake.
❖Maana ya kushuhudia "kuwa Muhammadi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu":
Kuitakidi kuwa Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, aliyetumwa kuwa wa mwisho wa Manabii, hivyo hakuna nabii baada yake, na ni juu yetu kumtii katika yale aliyotuamrisha, na kujiepusha na kila alichotukataza kukifanya.
2- Kutekeleza swala:
Mwenyezi Mungu amewajibisha juu yetu tumuabudu kwa Swala katika kila siku mara tano katika nyakati maalumu, na Swala hii ina masharti na namna ili iwe yenye kukubaliwa, na ametujulisha sifa zake Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani ziwe juu yake.
Na swala za wajibu kwa Muislamu ni swala tano usiku na mchana, nazo ni: Sala ya Al-fajir, na Sala ya Adhuhuri, na Sala ya Al-asri, na Sala ya Magharibi, na Sala ya Ishaa.
3- Zaka:
Ameamrisha Mwenyezi Mungu Zaka kwa kila Muislamu tajiri ili kuupima ukweli wa imani yake, na kumshukuru Mola wake Mlezi kwa kumneemesha neema ya mali, na kuwasaidia masikini na wenye kuhitajia, na kuwapa msaada katika mambo ya maisha yao. Na kutoa zaka kunakuwa kwa kuwapa watu wenye kustahiki, na hakika aya nyingi katika Qur'ani zimeashiria kwenye wito wa kutoa zaka [1].
▪Nayo ni haki ya wajibu katika mali itakapokuwa imefikia kiwango maalumu, hupewa aina nane alizozitaja Mwenyezi Mungu katika Qur'ani tukufu, miongoni mwao ni mafukara na masikini. [1] Mwenyezi Mungu amesema katika Qur'ani: "Na shikeni Swala, na toeni Zaka, na inameni pamoja na wanaoinama." [Al-Baqarah:43].
▪ Na katika kuitekeleza kwake kuna kusifika kwa sifa ya huruma na upole, na kusafisha tabia za Muislamu na mali yake, na kuziridhisha nafsi za mafukara na masikini, na kuzidisha mapenzi na udugu kati ya Waislamu; na kwa hivyo Muislamu mwema huitoa zaka kwa moyo safi na kufurahia utekelezaji wake, kwa sababu kutoa zaka ni kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kunafurahisha watu wengine.
▪Na kiwango cha zaka ya mali ni 2.5% katika mali iliyolimbikizwa miongoni mwazo ni Dhahabu na fedha, na pesa tasilim na bidhaa za biashara zilizo andaliwa kwa ajili ya kuuza na kununua ili kupata faida; zinapofikia thamani yake kiwango maalumu, na zikazungukiwa na mwaka mzima.
▪Kama ambavyo ni wajibu kutoa zaka kwa mwenye kumiliki idadi maalumu ya wanyama wafugwao (Ngamia, Ng'ombe, na Mbuzi), ikiwa wanakula majani ya malishoni mwaka mzima pasina kulishwa na mmiliki wa wanyama.
▪Na hivyo hivyo ni wajibu kutoa zaka kwa kinachotoka katika ardhi miongoni mwa nafaka na matunda ikiwa zitafikia kiwango maalumu, na hilo ni wakati wa kuvunwa kwake na kuchumwa matunda yake.
4- Swaumu:
Mwenyezi Mungu amefaradhisha kwa Waislamu kufunga mwezi mmoja katika mwaka, nao ni mwezi mtukufu wa Ramadhani, na akaufanya kuwa Nguzo ya Nne miongoni mwa nguzo za Uislamu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Saumu, kama walivyoandikiwa (watu) waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu." [Al-Baqara: 183].
❖Mwezi wa Ramadhani:
Ni mwezi wa tisa katika miezi ya mwandamo ya mpangilio wa kalenda ya Kiislamu, nao ni mwezi bora katika miezi ya mwaka, Mwenyezi Mungu ameufanya wa kipekee tofauti na miezi mingine kwa fadhila nyingi.
●Kwani ndani yake iliteremshwa Qur'ani tukufu kwa Mtume -rehema na amani ziwe juu yake. Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Mwezi wa Ramadhani ndio ambao imeteremshwa Qur-ani ndani yake kuwa uongofu kwa watu..." [Al Baqara: 183].
● Kwamba atakayefunga mchana wake na akasimama usiku wake katika swala; Mwenyezi Mungu atamsamehe madhambi yake yaliyotangulia. Amesema Mtume Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani: "Atakayefunga Ramadhani kwa imani na kwa kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia." [Imepokelewa na Bukhari], Na alisema Mtume Muhammad rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Atakayesimama Ramadhani kwa imani na kwa kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia." [Imepokelewa na Bukhari].
❖ Ufafanuzi wa Saumu:
Kufunga: Saumu Ni kumuabudu Mwenyezi Mungu, kwa kujizuia kula na kunywa na vyote vyenye kubatilisha swaumu, kuanzia kuchomoza kwa alfajiri mpaka kuzama jua.
❖Hukumu ya Funga:
Kufunga mwezi wa Ramadhani ni wajibu kwa kila Muislamu, aliyetimiza masharti ya ulazima wa kufunga.
❖Masharti ya kufunga:
Uislamu, kubalehe, akili timamu, uwezo wa kufunga, na kutokuwepo kwa kizuizi cha kisheria.
❖Mambo yanayobatilisha Funga:
Kula na kunywa kwa makusudi, na kufanya tendo la ndoa, na hedhi, na damu ya uzazi, na kujichua, na chochote kinachotolewa tumboni kwa makusudi kama vile kutapika.
Wala hafungui aliyesahau akala au kunywa; kwa kauli ya Mtume Muhammad rehema na amani ziwe juu yake: "Atakayesahau hali ya kuwa kafunga akala au akanywa, basi atimize swaumu yake, kwani Mwenyezi Mungu kamlisha na kamnywesha." [Imepokelewa na Muslim].
5- Kuhiji Nyumba Tukufu:
Mwenyezi Mungu amewajibisha kwa kila Muislamu mwanamume na mwanamke kwenda Makkah kwa ajili ya kuhiji Nyumba yake tukufu mara moja katika umri, na kwenda huku kunakuwa kwa mwenye uwezo na akaweza, na wajibu wa Hija unaondoka kwa kila Muislamu asiyekuwa na uwezo wa kwenda, sawa uwe ni wa mali au wa afya.
Na katika Hija anapitisha Muislamu idadi ya siku katika Makkah, anatekeleza ndani yake mkusanyiko wa ibada maalumu ambazo hazitekelezi muislamu yeyote isipokuwa katika Hija, nayo ni Ibada kubwa inamfundisha Muislamu subira, na kujivua kutokana na pambo la maisha ya dunia, na kujiandaa kukutana na Mwenyezi Mungu, na inaondoa tofauti kati ya watu.
Na kwa hivyo, ni nguzo tukufu ambayo kwayo Mwenyezi Mungu husamehe madhambi yote, na Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, ameashiria ya kwamba atakaekwenda katika Hija na akaitekeleza kama alivyomuamrisha Mwenyezi Mungu, anastahiki msamaha wa madhambi yake yote yaliyotangulia.
Somo la Tano:
Nguzo za Imani
Tumejifunza kuwa nguzo za Uislamu ni matendo ya wazi wazi anayoyatekeleza Muislamu katika maisha yake, na ama nguzo za imani ni matendo ya ndani anayoyaamini Muislamu na kuyasadikisha kwa moyo wake, na kupitia hayo Muislamu hujenga uhusiano wake na Mwenyezi Mungu, na ujuzi wake wa mambo ya ghaibu, na maisha ya Akhera.
Nayo inawakilisha asili ya itikadi ya Kiislamu ambayo walikuja nayo Manabii wote.
Nguzo sita za Imani ni:
1. Kumuamini Mwenyezi Mungu.
2. Kuamini Malaika.
3. Kuamini Vitabu vya mbinguni.
4. Kuwaamini Mitume.
5. Kuamini Siku ya Mwisho.
6. Kuamini hukumu na kadari.
1- Kumuamini Mwenyezi Mungu:
Na inajumuisha yafuatayo:
Maumbile yaliyo salama ni dalili wazi juu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu, basi sisi tukiiona meli, tunajua kuwa inamtengenezaji, na tukiuona ulimwengu huu mkubwa uliopangiliwa, tunajua kuwa una muumbaji Muweza Mwenye hekima.
Lakini mazingira, malezi na desturi yanaweza kuathiri maumbile haya, yakapotoka katika usawa wake, na kuelekeza ibada yake kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu.
• Muislamu anaamini kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mola Mlezi pekee wa ulimwengu huu: Na Yeye ndiye Muumba, na Mwenye kuruzuku, na Mwenye kuhifadhi, Mwenyezi Mungu ndiye Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na Mmiliki wa ulimwengu mzima, wala hakuna yeyote anayeshirikiana naye katika hilo.
Kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: Sema, "Ni nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini? Au ni nani anayemiliki kusikia na kuona? Na ni nani atoaye kilicho hai kutoka kwa maiti, na atoaye maiti kutoka kwa kilicho hai? Na ni nani anayeyaendesha mambo yote?" Basi watasema, "Mwenyezi Mungu." Basi sema, "Je, hamchi?" [Yunus: 31].
• Muislamu anaamini kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mtawala pekee wa viumbe vyote: Kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Fahamuni! Ni kwake kuumba na amri." [Surat Al-A'araf: 54]
• Muislamu anaamini kuwa Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kustahiki kuabudiwa pekee: Kuamini Uungu wa Mwenyezi Mungu na kuwa yeye ndiye anayestahiki kuabudiwa peke yake hana mshirika kwa chochote, ibada hizo ni kama vile swala, na dua, na ibada zingine zote, Kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Na Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, hapana mungu ila Yeye. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu." [Al-Baqarah: 163].
• Muislamu anaamini kwamba Mwenyezi Mungu pekee ndiye ana ukamilifu na majina mazuri zaidi na sifa za juu zaidi: Kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri kabisa, basi muombeni kwayo..." [Al-A'raf: 180].
• Kubwa zaidi katika mambo yanayotengua kumuamini Mwenyezi Mungu:
Ushirikina: Nako ni kushirikisha miungu mingine inayoabudiwa pamoja na Mwenyezi Mungu, na hakuna katika Uislamu dhambi kubwa zaidi kuliko kumshirikisha Mwenyezi Mungu. Nayo ni dhambi ambayo Mwenyezi Mungu haisamehi kamwe isipokuwa kwa kutubia kwake, na kudumu katika kumuabudu Yeye pekee mpaka mauti, kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Hakika, Mwenyezi Mungu hafuti dhambi ya kushirikishwa, na hufuta dhambi ya yasiyokuwa ushirikina kwa amtakaye. Na mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, basi hakika amezua dhambi kubwa." [An-Nisaa :48]
Na shirki ina aina nyingi, mfano: Kumuomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu na kumuomba dua amponye ugonjwa wake na amkunjulie riziki yake, au kumtegemea asiyekuwa Mwenyezi Mungu, au kumsujudia asiyekuwa Mwenyezi Mungu.
2- Kuamini Malaika:
Na inajumuisha yafuatayo:
• Kuamini uwepo wa Malaika, na kwamba wao ni miongoni mwa viumbe wa Mwenyezi Mungu: Muislamu anaamini ya kwamba Malaika ni viumbe halisia, walioumbwa, lakini wamekingwa na hisia zetu, wala hawana sifa za Uungu, nao ni viumbe ambao Mwenyezi Mungu aliwaumba kutokana na nuru kabla ya wanadamu, na miongoni mwa sifa zao ni kuwa wao hawali wala hawanywi, Mwenyezi Mungu amewajalia nguvu kubwa mno na kasi kubwa sana katika kutekeleza amri zake, na hakuna ajuaye idadi yao ila Mwenyezi Mungu.
• Kuamini kuwa wao hawastahiki aina yoyote ya ibada.
• Kuamini majina na matendo aliyoyabainisha Mwenyezi Mungu kwa kila mmoja wao: Miongoni mwa Malaika kuna aliyepewa jukumu la kushuka kwa mvua, na miongoni mwao kuna aliyepewa jukumu la kutoa roho katika miili wakati wa kufa, naye ni Malaika wa mauti. Mwenyezi Mungu amesema katika Qur'ani: "Sema, "Atakufisheni Malaika wa mauti aliyewakilishwa juu yenu; kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu Mlezi."" [As-Sajda: 11], Na Malaika kwa ujumla wana kazi nyingine ambazo hakuna anayejua aina zake na idadi zake isipokuwa Mwenyezi Mungu.
3- Kuamini Vitabu vilivyoteremshwa:
Na inajumuisha yafuatayo:
• Kuamini kwamba Mwenyezi Mungu aliteremsha Vitabu kwa Manabii: Muislamu huamini kuwa Mwenyezi Mungu ameteremsha Vitabu vya mbinguni kwa Manabii wake ili kuwaongoza watu na kuwafundisha njia ya kheri na haki, kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Amekiteremsha Kitabu juu yako kwa haki, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake. Na aliteremsha Taurati na Injili. Kabla yake, viwe uongofu kwa watu..." [Al Imran: 3-4].
Na Muislamu huamini kuwa Mwenyezi Mungu ameteremsha Qur'ani kwa Mtume Muhammad -rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani-, na kuwa yeye ameteremsha vitabu vingine kwa Manabii kabla yake, miongoni mwa vitabu hivyo ni Taurati: iliyoteremshwa kwa Musa amani iwe juu yake, (nayo inatofautiana na "Agano la Kale" linalotumika leo), na Injili: iliyoteremshwa kwa Isa amani iwe juu yake (nayo inatofautiana na "Agano Jipya" lililopo sasa), na Zaburi: iliyoteremshwa kwa Daudi amani iwe juu yake. Na huamini Nyaraka za Ibrahim na Musa, na Muislamu huamini kuwa vitabu hivyo vina maneno ya Mwenyezi Mungu, lakini vimebadilishwa isipokuwa Qur'ani, Ufunuo wa mwisho kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Hakika Sisi ndio tuliouteremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutakaoulinda." [A Hijri: 9].
Qur'ani ni nini?
Hicho ni kitabu cha Mwenyezi Mungu alichokiteremsha kwa Nabii wake wa mwisho Muhammad -rehema na amani ziwe juu yake- kwa ufunuo kwa njia ya Jibril amani iwe juu yake, nacho kimehifadhiwa kutokana na kubadilishwa au kugeuzwa, na Waislamu hufanya ibada kwa kukisoma, nacho ndio chanzo cha kwanza cha sheria, na ndani yake kuna visa vya umati uliotangulia na habari za Kiyama, na miongozo na nasaha kwa wanadamu.
Na Qur'ani imeteremka kwa lugha ya Kiarabu, na Waislamu wamejitahidi kutafsiri maana yake kwenda katika lugha za ulimwengu; ili kila Muislamu afaidike nayo kulingana na lugha yake.
❖ Kuamini Qur'ani, kunaingia ndani yake vipengele kadhaa:
• Kuamini kuwa ni miongoni mwa vitabu vya Mwenyezi Mungu, na kuamini kuwa ni muujiza unaobakia wa Nabii Muhammad - rehema na amani ziwe juu yake.
• Kuamini kuwa ni chanzo cha msingi cha Uislamu.
• Kuamini kuwa ni kitabu cha mwisho cha mbinguni, na kwamba Mwenyezi Mungu hatateremsha kitabu kingine baada yake.
• Kuamini kuwa kila kilichomo katika Qur’ani ni haki, hakuna batili ndani yake wala shaka.
• Kuamini kwamba Qur'ani imehifadhiwa, haijabadilika wala haitabadilika.
4- Kuwaamini Mitume:
Na inajumuisha yafuatayo:
Kuamini Mitume maana yake ni: Kusadiki kuwa Mwenyezi Mungu alichagua watu wema ili wawaite watu katika njia ya haki, na haki kubwa zaidi ni kumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na kuwaonya dhidi ya batili, na batili kubwa zaidi ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu, pia aliwatuma ili wawabainishie wanadamu lengo la kuwepo kwao katika maisha haya, ili yeyote asibakiwe na udhuru mbele ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama.
• Mwenye kumkufuru Mtume mmoja, basi ni kama amewakufuru Mitume wengineo wote: Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Qur'ani kuhusu watu wa Nuhu, pamoja na kuwa hakutumwa kwao isipokuwa Nuhu: "Kaumu ya Nuhu waliwakadhibisha Mitume." [Ash-Shu'ara: 105] Yaani: mwenye kumkadhibisha Mtume mmoja, basi hakika amewakadhibisha wote.
• Kuwaamini Manabii wote waliotajwa na wasiotajwa:
Tunawaamini wale aliowataja majina yao Mwenyezi Mungu, kama vile: Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake, Ibrahim, Musa, Isa, na Nuhu - amani iwe juu yao, na wale ambao majina yao na visa vyao havikutajwa.
Kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Na bila ya shaka tuliwatuma Mitume kabla yako. Wengine katika hao tumekusimulia habari zao, na wengine hatukukusimulia." [Ghafiri: 78].
• Kuamini kuwa Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake, ndiye mwisho wa Manabii na hakuna Nabii baada yake; kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii..." [Al-Ahzab: 40].
• Kumfuata Mtume Muhammad rehema na amani ziwe juu yake na kuamini ya kwamba yeye ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwa wanadamu wote, na kwamba mafundisho yake yamehifadhiwa, kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Na anachokupeni Mtume, kichukueni. Na anachokukatazeni, jiepusheni nacho." [Al-Hashr: 7]
• Manabii ni watu na sio miungu:
Wao ni waja wema tu, na Mitume wa Mwenyezi Mungu, wanafikisha yale aliyowaamrisha, na walikuwa wakila na wakinywa na wakilala na wakiugua na wakifa.
Na hawana elimu ya ghaibu isipokuwa kile alichowafunza Mwenyezi Mungu, wala hawasamehe dhambi, wala hawana ushiriki wowote katika uendeshaji wa ulimwengu, na miujiza yao yote haitoki kwao, bali ni kwa idhini ya Mola wao Mlezi.
5- Kuamini Siku ya Mwisho:
Na inajumuisha yafuatayo:
Kuamini kwamba itakuja siku ulimwengu huu utatoweka, na ulimwengu mpya utachukua nafasi yake, ulimwengu ambao Mwenyezi Mungu atawafufua ndani yake viumbe, na kuwahesabu juu ya matendo yao, basi atakayeamini ataingia katika Pepo ya Adni milele, na atakayekufuru ataingia katika moto wa Jahannamu milele.
6- Kuamini hukumu na kadari:
Na inajumuisha yafuatayo:
• Kuamini kwamba elimu ya Mwenyezi Mungu imeenea katika kila kitu:
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Hakika, Mwenyezi Mungu hakifichikani chochote kwake, katika dunia wala katika mbingu." [Al-Imran: 5]
• Kuamini kwamba Mwenyezi Mungu alikwishaandika kila kitu kitakachotokea hadi Siku ya Kiyama katika kitabu kinachojulikana kama "Ummul Kitab" au "Lauhul Mahfudh".
Na inamaanisha: kwamba Mwenyezi Mungu aliandika ndani yake kila kitu kitakachotokea, tangu mwanzo wa uumbaji mpaka kusimama Kiyama.
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Je, hujui kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na katika ardhi? Hakika hayo yamo Kitabuni. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi." [Al-Hajj: 70]
• Kuamini kuwa kila alichotaka Mwenyezi Mungu kilikuwa, na kinatokea, na kitatokea, hakitokei kitu kinyume na matashi yake au bila ya hayo, na vilevile vitendo vya viumbe vinatokea kwa matakwa yake:
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Wala nyinyi hamtataka isipokuwa atake Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote." [At-Takwir: 29].
• Kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ni muumba wa kila kitu:
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi, Muumba wa kila kitu..." [Surat Ghafir: 62]
• Utashi wa kibinadamu na Uhuru:
Mwanadamu si kiumbe wa kulazimishwa, na ana uhuru wa kuchagua unaohitajika ili awe mbebaji wa majukumu ya matendo yake, lakini hautoki nje ya matashi ya Mwenyezi Mungu.
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Basi na atakaye, aamini. Na atakaye, akufuru." [Al-Kahf: 29]
Somo la Sita:
Twahara
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Hakika, Mwenyezi Mungu huwapenda wanaotubu, na huwapenda wanaojisafisha." [Al-Baqara: 222].
Na miongoni mwa utukufu wa swala ni kuwa Mwenyezi Mungu ameweka sheria ya kujisafisha kabla yake, na akafanya twahara (usafi) kuwa ni sharti la kukubalika swala, na twahara ndiyo ufunguo wa swala, na kuvuta hisia ya utukufu wake kunaufanya moyo uwe na shauku ya kutekeleza swala. Na kwa hakika ametueleza Mtume (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) kuwa Muislamu anapotawadha kwa ajili ya swala udhu ulio sahihi, hakika dhambi zake alizozitenda zinamuondoka, kama vile maji aliyotawadhia yanavyoondoa uchafu ulioko kwenye uso wake na mikono yake na miguu yake anapoiosha, hivyo mja humwelekea Mola wake Mlezi akiwa amejitwaharisha twahara ya kihisia kwa udhu, na ya kimaana kwa kujitwaharisha kwake kutokana na dhambi zake, akiwa mwenye kumtakasia nia Mwenyezi Mungu, na mwenye kufuata mwongozo wa Mtume (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake).
Yanayopaswa kufanywa ukiwa na Udhu:
● Swala ya aina yoyote sawa iwe ya Faradhi au iwe ya Sunna.
● Kutufu Al-Kaaba (nyumba tukufu)
● Kushika Msahafu.
Miongoni mwa masharti ya udhu:
1- Nia:
Na mahala pake ni moyoni, na maana ya nia: Ni kuazimia moyoni kufanya ibada, kwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.
2- Maji Twahuru (Masafi mno):
Maji safi: ni kila maji yaliyoteremka kutoka mbinguni, au yakachimbuka kutoka ardhini, na yakabakia katika asili ya umbile lake, na hayakubadilika moja kati ya sifa zake tatu, nazo ni: rangi, ladha, na harufu.
Namna ya kutawadha:
1. Atasema 'Bismillaah (Kwa jina la Mwenyezi Mungu).'
2. Ataosha viganja vyake viwili kwa maji, na inapendekezwa kwake kufanya hivyo mara tatu.
3. Asukutue kwa maji, kwa maana: kuingiza maji katika kinywa chake na kuyatikisa kwa ndani kisha kuyatoa nje, na inapendekezwa kwake kufanya hivyo mara tatu, na wajibu ni mara moja.
4. Apandishe maji puani, kwa maana: kuyavuta maji kwa pua yake kisha kuyatoa kwa kuyapenga, yaani: kuyasukuma maji nje kwa msukumo wa hewa inayotoka puani, na inasuniwa kwake kubalighi isipokuwa ikiwa hilo litamsababishia madhara au akiwa amefunga, na ni sunna kwake kukariri hilo mara tatu, na wajibu ni mara moja.
5. Aoshe uso wake, nao ni kutoka juu ya paji la uso kuanzia maoteo ya nywele hadi chini ya kidevu, na kutoka sikio hadi sikio, na masikio mawili hayaingii katika uso, na inapendekezwa kwake kufanya hivyo mara tatu, na wajibu ni mara moja.
6. Aoshe mikono yake miwili kuanzia ncha za vidole vyake mpaka katika viwiko viwili, na viwiko viwili vinaingia katika kuosha, na ni Sunna kwake kurudia hilo mara tatu, na wajibu ni mara moja.
7. Apanguse kichwa chake kwa kuloanisha mikono yake kwa maji kisha apanguse juu ya kichwa chake kuanzia mbele ya kichwa mpaka mwisho wa kichwa katika sehemu inayofuatia shingo, na inasuniwa kwake kuirejesha mikono yake akipangusa mpaka mbele ya kichwa mara nyingine, na haipendekezwi kurudia kufanya hivyo mara tatu kama ilivyo katika viungo vingine.
8. Atapaka maji masikio yake kwa kuingiza vidole vyake viwili vya shahada ndani ya masikio yake baada ya kupaka maji kichwa chake, na atapaka kwa vidole gumba nje ya masikio mawili.
9. Ataosha miguu yake miwili pamoja na fundo mbili, na ni Sunna kurudia hilo mara tatu, na wajibu ni mara moja.
Vyenye kuharibu Udhu:
● Kile kinachotoka katika njia mbili: kama mkojo, na haja kubwa, na upepo, na manii, na madhii.
● Kuondokwa na akili kwa kulala usingizi au kuzimia, au kulewa, au kupatwa na wenda wazimu.
●Kila chenye kulazimisha kuoga: kujamiana, na hedhi, na nifasi.
Tanbihi: Mwanadamu akikidhi haja yake, anapaswa kuondosha najisi, ima kwa maji safi (na hii ndiyo njia bora zaidi), au pasina kutumia maji safi kwa vitu vinavyoondosha najisi kama tishu, na mawe au karatasi au vitambaa na vinginevyo vinavyoiondosha, na kwa sharti iwe kuondoa huko ni kwa kufuta mara tatu au zaidi kwa kitu chenye kutakasa na kilicho safi na halali kukitumia.
Hadathi kubwa inayolazimisha kuoga:
❖Mwenye Janaba:
Ikitokea kwa mwanamume au mwanamke kitendo cha kujamiiana, au yakatoka manii wakiwa katika hali ya kuamka au kulala; ni wajibu juu yao kuoga kabla ya kuanza kutekeleza swala au kufanya mambo ambayo yanalazimu twahara.
❖ Twahara kutokana na hedhi na nifasi:
Mwanamke akitwaharika kutoka kwenye hedhi na nifasi ni wajibu kwake kuoga kabla ya kuanza kutekeleza swala au kufanya mambo ambayo yanalazimu twahara.
• Namna ya Kuoga:
Aueneze Muislamu mwili wake wote kwa maji kwa njia yoyote ile pamoja na kusukutua na kuingiza maji puani, akiwa amenuia kuoga.
Hutahadharishwa mwenye janaba kufanya mambo yafuatayo mpaka aoge:
● Swala.
● Kutufu Al-Kaaba (Nyumba tukufu)
● Kukaa msikitini, na yafaa kwake kupita tu pasi na kukaa.
● Kushika Msahafu.
● Kusoma Qur'ani.
Attayammum:
Ikiwa Muislamu hajapata maji ambayo atajitwaharishia, au hakuweza kuyatumia maji kutokana na maradhi au madhara na mfano wake, na akahofia usimpite wakati wa swala, basi atatayamamu kwa kutumia udongo.
• Namna ya kutayammamu:
Na namna yake: Ni apige kwa mikono yake miwili juu ya udongo pigo moja, kisha apake kwa mikono hiyo uso wake na viganja vyake tu. Na ni sharti udongo uwe twahara.
• Mambo yanayoharibu Kutayammamu:
- Huharibika tayamamu kwa kila chenye kuharibu udhu.
- Yakipatikana maji kabla ya kuanza ibada ambayo ametayamamu kwa ajili yake.
Somo la Saba:
Kufundisha Swala
Amemfaradhishia Mwenyezi Mungu Muislamu swala tano usiku na mchana, na akaziwekea nyakati dhahiri, nazo ni: Al-fajiri, na Adhuhuri, na Alaasiri, na Magharibi, na Ishaa.
1- Sala ya Alfajir :
Nayo ni rakaa mbili, na wakati wake huanza kuanzia kuchomoza Alfajiri, ambako ni mwanzo wa nuru katika upeo wa macho, na humalizika kwa kuchomoza kwa jua.
2- Sala ya Adhuhuri:
Nayo ni rakaa nne, na wakati wake unaanza kuanzia kupinduka kwa jua mchana, na unamalizika kitakapofikia kivuli cha kila kitu sawa na urefu wake.
3- Sala ya Alasiri:
Nayo ni rakaa nne, na wakati wake unaanza kuanzia kutoka wakati wa Adhuhuri pindi kivuli cha kila kitu kinapokuwa sawa nacho, na unamalizika kwa kuzama kwa jua, na inampasa Muislamu kuharakisha swala kabla miale ya jua haijadhoofika na rangi yake kuwa njano.
4- Sala ya Magharibi:
Nayo ni rakaa tatu, na wakati wake unaanza kuanzia kuzama Jua na kutoweka kwa duara lake katika upeo wa macho, na unamalizika kwa kuzama wingu jekundu linaloonekana baada ya kuzama.
5- Sala ya Ishai:
Nayo ni rakaa nne, na wakati wake unaanza kuanzia kutoweka kwa mawingu nyekundu, na unamalizika katikati ya usiku, na inawezekana kuiswali wakati wa dharura mpaka kuchomoza Alfajiri.
Tanbihi: Muislamu anaweza kutegemea kalenda zinazoonyesha nyakati za swala kwa kila mji.
Kujiandaa kwa ajili ya swala:
Ukiingia muda wa swala, atajitwaharisha Muislamu kutokana na hadathi (Uchafu) mdogo na mkubwa, ikiwa kapatwa na hadathi kubwa.
Na hadathi kubwa ni: Kila kinachomlazimisha Muislamu kuoga.
Hadathi ndogo ni: Kila kinachomlazimisha Muislamu kutawadha.
- Husali Muislamu akiwa katika twahara na katika sehemu safi kutokana na najisi, akiwa ameusitiri uchi wake.
- Anajipamba Muislamu kwa mavazi yanayofaa wakati wa swala na husitiri kwa mavazi hayo mwili wake, na haifai kwa mwanamume wakati wa kuswali aache wazi sehemu yoyote kuanzia sehemu ya kitovuni mpaka magotini.
- Ni wajibu kwa mwanamke kuusitiri mwili wake wote ndani ya swala, isipokuwa uso na viganja viwili.
- Hazungumzi Muislamu akiwa katika swala maneno yasiyokuwa maalumu kwa ajili ya swala.
Namna ya kuswali:
1- Nia:
Na mahala pake ni moyoni, na maana ya nia: Ni kuazimia moyoni kufanya ibada kwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.
2- Udhu (kutawadha).
3- Kuelekea kibla:
Nayo ni mwenye kuswali aelekee Makka, na anaweza kubainisha muelekeo kwa kutumia dira, au njia nyinginezo.
4- Kuswali akiwa amesimama kwa yule anayeweza kufanya hivyo.
5- Takbira:
Kuinua mikono miwili usawa wa mabega mawili na kusema: 'Allahu Ak-baru (Mwenyezi Mungu ni Mkubwa), huku akinuia kuingia katika swala.
6- Kusoma Suratul Faatiha katika kila rakaa:
Nayo ni: "1. Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. 2. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu. 3. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. 4. Mmiliki wa Siku ya Malipo. 5. Ni Wewe tu tunayeabudu, na ni Wewe tu tunayeomba msaada. 6. Tuongoze njia iliyonyooka. 7. Njia ya wale uliowaneemesha. Siyo ya wale waliokasirikiwa, wala waliopotea." [Suratul- Faatiha 1-7].
Kusoma kilicho chepesi kwenye Qur'ani baada ya Suratul Faatiha katika rakaa ya kwanza na ya pili tu katika kila swala, na kusoma huku siyo lazima, lakini kufanya hilo kuna malipo makubwa.
7- Rukuu:
Kusema: 'Allahu Akbaru (Mwenyezi Mungu ni Mkubwa)', kisha kurukuu mpaka unakuwa mgongo umelingana sawa, na mikono miwili inakuwa juu ya magoti mawili, kisha kusema katika kurukuu: “Sub-haana rabbial Adhwiim (Ametakasika Mola wangu Mtukufu)."
8. Kunyanyuka kutoka katika rukuu:
Kunyanyuka kutoka katika rukuu akisema: "Sami'allaahu liman hamidah (Amemsikia Mwenyezi Mungu mwenye kumhimidi)", huku akinyanyua mikono usawa wa mabega mawili, na wakati wa kusimama sawa sawa mwili pamoja na kusema: "Rabbanaa walakal-hamdu (Mola wetu Mlezi, sifa njema ni zako)".
9- Sijida:
Kusema: "Allaahu Akbar (Mwenyezi Mungu ni Mkubwa)" pamoja na kusujudu kwa mikono miwili na magoti mawili na miguu miwili na paji la uso na pua, na kusema katika sijida: "Sub-haana rabbial a'laa (Ametakasika Mola wangu Mlezi aliye juu)."
10- Kukaa kati ya sijida mbili:
Kusema: Allahu Akbaru (Mwenyezi Mungu ni Mkubwa), kisha kuinuka kutoka kwenye kusujudu mpaka mgongo unalingana sawa hali ya kunyooka, pamoja na kukalia mguu wa kushoto na kuusimamisha mguu wa kulia, na kusema: "Rabbigh-firli (Ewe Mola wangu Mlezi, nisamehe)."
11- Sijida ya pili:
Kusema: "Allahu Akbaru (Mwenyezi Mungu ni Mkubwa)" na kusujudu mara nyingine tena mfano wa sijida ya kwanza.
12- Rakaa ya pili:
Kunyanyuka kutoka katika sijida pamoja na kusema: "Allahu Ak-baru" mpaka mgongo uwe sawa akiwa amesimama, na atafanya katika rakaa za swala zilizobakia kama alivyofanya katika rakaa ya kwanza.
Baada ya rakaa ya pili ya swala ya Adhuhuri na Alasiri, na Magharibi, na Ishaa, atakaa kwa ajili ya kusoma tahiyatu ya kwanza, nayo ni: 'Attahiyyaatulillahi, Wasswalawaatu wattwayyibaatu. Assalaamu alaika Ayyuha Nabiyyu Warahmatullahi Wabarakaatuhu. Assalaamu alaina wa'alaa ibadillahi sswaalihiina. Ash-hadu an-laailaaha illa llahu wa anna Muhammadan abduhu wa rasuulullahi (Maamkizi yote ni ya Mwenyezi Mungu, na swala zote na mema yote. Amani iwe juu yako ewe Mtume, na rehema za Mwenyezi Mungu na baraka zake. Amani iwe juu yetu na juu ya waja wema wa Mwenyezi Mungu. Nashuhudia kuwa hakuna mungu apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu, na nashuhudia kuwa Muhammad ni mja wake na Mtume wake)', kisha atasimama kwa ajili ya rakaa ya tatu baada ya hapo.
Baada ya rakaa ya mwisho ya kila swala ni wajibu kukaa kwa ajili ya kusoma tahiyatu ya mwisho, nayo ni: "Attahiyyaatulillahi, Wasswalawaatu wattwayyibaatu. Assalaamu alaika Ayyuha Nabiyyu Warahmatullahi Wabarakaatuhu. Assalaamu alaina wa'alaa ibadillahi sswaalihiina. Ash-hadu an-laailaaha illa llahu wa anna Muhammadan abduhu wa rasuulullahi. Allahumma swalli alaa Muhammadin wa'alaa aali Muhammadin, kamaa swallaita alaa ibrahiima wa'alaa aali ibrahiima Innaka hamiidun majiid, Allahumma baariki alaa Muhammadin wa alaa aali Muhammadin, kamaa baarakta alaa ibraahiima wa- alaa aali ibrahiima innaka hamiidun majiid" Tafsiri yake: Maamkizi (Amani) ni ya Mwenyezi Mungu, na swala na vile vilivyo vizuri, amani iwe juu yako ewe Nabii na rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka zake, amani iwe juu yetu na juu ya waja wema wa Mwenyezi Mungu, nashuhudia kuwa hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu, na ninashuhudia kuwa Muhammadi ni mja wake na ni mjumbe wake. Ewe Mwenyezi Mungu mpe rehema Muhammad na watu wa Muhammad, kama ulivyompa rehema Ibrahim na watu wa Ibrahim, hakika Wewe ni Msifiwa, Mwenye utukufu, ewe Mwenyezi Mungu mbariki Muhammad pamoja na watu wa Muhammad kama ulivyombariki Ibrahim na watu wa Ibrahim, hakika Wewe ni Msifiwa, Mwenye utukufu.
13- Kutoa salamu:
Baada ya hapo atageuka mwenye kusali upande wa kulia pamoja na kusema: "Assalaam alaikum warahmatullahi (Amani iwe juu yenu na rehema za Mwenyezi Mungu)", kisha upande wa kushoto pamoja na kusema: "Assalaam alaikum warahmatullahi", pamoja na nia ya kutoka ndani ya swala, na kwa kufanya hivyo swala inakuwa imekamilika.
Somo la Nane:
Kuhifadhi Suratul Fatiha na Suratul Ikhlaswi
Suratul Fatiha:
Tafsiri:
"Alhamdulillaah": Ni kumsifu kikamilifu Mwenyezi Mungu pekee kwa sifa za ukamilifu alizo nazo, na kwa neema zake za dhahiri na za siri.
"Mola Mlezi wa walimwengu" Yeye ni Muumba wa kila kitu, na anayepangilia mambo yao.
Aya ya 3: "Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu."
Tafsiri:
"Ar- rahmaan" Mwenye rehema pana ambayo imekusanya kila kitu.
"Mwenye kurehemu" Mwenye rehema maalumu kwa Waumini katika dunia na Akhera.
• Aya ya 4: "Mmiliki wa Siku ya Malipo."
Tafsiri:
"Maliki" Mmiliki wa kitu ndiye muendeshaji wake yeye peke yake, wala hana mshirika yeyote.
"Siku ya Malipo" ni Siku ya Kiyama, ambayo kila mtu atalipwa kwa mujibu wa matendo yake.
Tafsiri:
"Ni Wewe tu tunayeabudu" yaani tunakuhusisha Wewe peke yako kwa ibada na hatumuabudu asiyekuwa Wewe.
"Na ni Wewe tu tunayeomba msaada" na tunataka msaada kwako peke yako katika mambo yetu yote.
• Aya ya 6: "Tuongoe kwenye njia iliyonyooka."
Tafsiri:
"Tuongoe" yaani tuonyeshe na utuwezeshe na utuimarishe juu ya haki.
"Njia iliyonyooka" Njia iliyo wazi ambayo inafikisha kwenye radhi za Mwenyezi Mungu na Pepo yake.
Tafsiri:
"Njia ya wale uliowaneemesha" Njia ya wale uliowaneemesha miongoni mwa Manabii na wema.
"Si ya wale waliokasirikiwa" Wale walioijua haki na wakaiacha.
"Wala waliopotea" ambao wamepotea kutoka kwenye haki kwa sababu ya ujinga au upotovu.
Suratul Ikhlaswi:
• Aya ya 1: "Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni wa Pekee."
Tafsiri:
"Sema" Tangaza na fikisha haki hii.
"Mwenyezi Mungu ni wa Pekee" Mwenyezi Mungu ni Mmoja katika Dhati yake, Majina yake, Sifa zake na Matendo yake, hana mshirika.
• Aya ya 2: "Mwenyezi Mungu ndiye Mkusudiwa."
Tafsiri:
Aliyekamilika katika sifa zake, ambaye anakusudiwa katika haja zote, asiyehitajia viumbe wake, na viumbe wote wanahitajia kwake.
• Aya ya 3: "Hakuzaa wala hakuzaliwa."
Tafsiri:
"Hakuzaa" Hana mtoto.
"Wala hakuzaliwa" na wala hakuzaliwa na yeyote; kwa sababu Yeye ni Mkamilifu, anayejitosheleza asiyehitaji wengine.
• Aya ya 4: "Wala hana anayelingana naye hata mmoja."
Tafsiri:
Hana mwenye kufanana naye wala mfano wake katika dhati yake au sifa zake au vitendo vyake.
Somo la Tisa:
Dhana ya ibada
Ibada katika Uislamu:
Nayo ni jina la yale yote anayoyapenda Mwenyezi Mungu na kuyaridhia katika maneno na matendo ya wazi na ya siri.
Basi kila kauli au kitendo kinachokusudiwa kupata malipo kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kuafikiana na yale aliyoyaweka kisheria Mwenyezi Mungu katika kitabu chake, au kupitia ulimi wa Mtume wake Muhammad, rehema na amani zimshukie, basi hiyo ni Ibada.
Aina za Ibada:
● Kuitakidi kwa moyo: Nako ni kusadikisha yale aliyoyatolea habari Mwenyezi Mungu kuhusu nafsi yake, na kuhusu majina yake, na sifa zake, na vitendo vyake, na kuamini Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Mwisho.
●Kauli kwa ulimi: Mfano kama kutamka shahada mbili, na kumtaja Mwenyezi Mungu, na kulingania kwake, na kubainisha haki.
● Matendo ya moyo: Mfano kama kumuhofu Mwenyezi Mungu, na kuwa na matarajio kwake, na kumpenda, na kutakasa nia katika matendo, na nayo ni miongoni mwa matendo tukufu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu.
● Kutenda kwa viungo: Mfano kama swala, na kufunga, na zaka, na kuwatendea wema watu, na matendo mema mengineyo.
Kwanza: Sharti za kukubalika kwa ibada:
Katika Uislamu, ibada haikubaliki kwa Mwenyezi Mungu isipokuwa ikikamilisha masharti mawili ya msingi:
1- Kutakasa matendo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu:
Yaani: Muislamu akusudie kwa ibada yake radhi za Mwenyezi Mungu peke yake, wala asitake kwayo sifa za watu au faida za kidunia. Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini..." [Al-Bayyina: 5]
2- Kumfuata Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake:
Yaani ibada iwe kwa namna ambayo ameelekeza Mtume Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, bila ya kuzidisha au kupunguza au kuzua, na yale aliyoyaelekeza hakika ni kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Mwenye kumtii Mtume, basi hakika amemtii Mwenyezi Mungu..." [An-Nisaa: 80]
Somo la Kumi:
Isa na Mariamu katika Uislamu
Waislamu wanawaamini Isa na Maryam - amani iwe juu yao - kwa imani kubwa, nao wanawapenda na kuwaheshimu kama Mwenyezi Mungu alivyotuamrisha, kama wengineo miongoni mwa Manabii na Mitume.
Na wanaamini kwamba Isa ni mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Mwenyezi Mungu alimtuma kwa ajili ya kuwaongoza watu, na kwamba Mariamu ni mwanamke msafi na mwenye kujihifadhi ambaye Mwenyezi Mungu alimchagua kwa muujiza mkubwa, ili awe ni ishara miongoni mwa ishara zake katika uumbaji wake na uwezo wake.
Ni nani Isa amani iwe juu yake:
Isa, amani iwe juu yake, ni Nabii na Mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na neno kutoka kwake alilompelekea Mariamu, yaani: kwamba Mwenyezi Mungu aliamrisha kuwepo kwake kwa neno kutoka kwake, basi akawa bila ya baba, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu pekee.
Mwenyezi Mungu alimtuma kwa Wana wa Israeli, akawa wa mwisho wa Manabii wao, naye ni mja wa Mwenyezi Mungu na mtume wake.
Na mama yake bikira Maryamu - amani iwe juu yake - Mwenyezi Mungu alimkhusisha kwa muujiza mkubwa; kwani alipata mimba ya Isa bila ya mwanamume kumgusa.
Kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Hakika, Masihi Isa mwana wa Maryam ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na neno lake tu alilomfikishia Maryam, na ni roho iliyotoka kwake. Basi Muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume wake.." [Suratun Nisaa: 171]
Isa amani iwe juu yake na miujiza yake:
Kuzaliwa kwa Isa, amani iwe juu yake, kulikuwa ni muujiza mkubwa, unaofanana na kuumbwa kwa Nabii Adam, amani iwe juu yake, zaidi kuliko wanadamu wengine, kwani aliumbwa bila ya baba, na alikuwa kwa neno kutoka kwa Mwenyezi Mungu alilolipeleka kwa Maryam.
Na hakika Mwenyezi Mungu amemkirimu kwa miujiza mingi, miongoni mwake ni kwamba alikuwa akiponya vipofu na wakoma kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na akiwafufua wafu kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na akiwaeleza watu kile wanachokula na wanachokiweka akiba katika majumba yao.
Na miujiza hii ilikuwa ni dalili ya ukweli wa ujumbe wake, na kwamba yeye ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na si mungu anayeabudiwa badala yake.
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Hakika, mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam. Alimuumba kwa udongo kisha akamwambia: 'Kuwa!' Basi akawa." [Al Imran: 59].
Na amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu kwa ulimi wa Isa amani iwe juu yake: "Mimi kwa hakika nimewajia na Ishara kutoka kwa Mola wenu Mlezi, ya kwamba mimi kwa hakika ninawaundia kwa udongo kama sura ya ndege. Kisha ninapuliza ndani yake na anakuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na ninawaponesha vipofu wa tangu kuzaliwa na wakoma, na ninawafufua maiti kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na ninawaambia mnachokila na mnachoweka akiba katika nyumba zenu.." [Al Imran: 49].
Jukumu la Isa amani iwe juu yake:
Jukumu la Isa, amani iwe juu yake, lilikuwa kama jukumu la Mitume waliokuwa kabla yake, Musa na Ibrahim -rehema na amani ziwe juu yao- na baada yake Muhammad, rehema na amani zimshukie, nalo ni kulingania katika kumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake asiye na mshirika, na kuacha ushirikina.
Basi Manabii wote walikuja na ujumbe mmoja, nao ni kwamba tumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, Muumba wa mbingu na ardhi, bila ya wapatanishi au washirika.
Na Isa (Yesu) amani iwe juu yake hakuja kudai kuwa yeye ni Mungu, au kusamehe kosa la Adam amani iwe juu yake; basi Uislamu unaeleza kuwa kila mwanadamu anabeba kosa lake mwenyewe, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu kwa yule anayetubia na kuamini.
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Na pale Mwenyezi Mungu aliposema: Ewe Isa mwana wa Maryamu! Je, wewe ndiye uliwaambia watu: Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu wawili badala ya Mwenyezi Mungu? (Isa) akasema: Subhanaka (Wewe umetakasika)! Hainifailii mimi kusema ambayo si haki yangu.." [Al Maaida: 116].
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu Mlezi, na Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye. Hii ndiyo njia iliyonyooka." [Al-Imran: 51].
Kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika kuthibitisha kwamba kila mwanadamu ndiye mbebaji wa majukumu ya matendo yake: "Na mbebaji hatabeba mzigo wa mwengine." [Faatwir: 18].
Kurudi kwa Isa amani iwe juu yake:
Waislamu wanaamini kwamba Isa - amani iwe juu yake - hakuuawa wala hakusulubishwa msalabani, bali Mwenyezi Mungu alimnyanyua kwenda kwake akiwa hai, na atateremka katika zama za mwisho, na atawabainishia watu ya kuwa yeye ni mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na atasimamisha uadilifu baina ya watu mpaka amani ienee.
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Na hawakumuua wala hawakumsulubisha, bali walifananishiwa tu." [Suratun Nisaai: 157]
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Qur'ani Tukufu: "Bali Mwenyezi Mungu alimwinua kwenda kwake, na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima." [An-Nisaa: 158].
Somo la kumi na moja:
Historia (Sira) ya Bwana Mtume.
Jina lake na ukoo wake:
Mtume Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake, ni Muhammad bin Abdallah bin Abdul Muttwalib, kutoka katika kabila la Makuraishi lililoko Makkah.
Alikuwa ni mbora wa Waarabu kwa tabia na sifa, na akajulikana kati ya watu wake kabla ya kupewa utume kwa ukweli na uaminifu, mpaka akaitwa kwa jina la mkweli muaminifu.
Mwenyezi Mungu alimtuma kwa wanadamu wote pamoja na tofauti za rangi zao, asili zao na matabaka yao.
Kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu nyinyi nyote..." [Al-A'araf: 158].
Na Mwenyezi Mungu alimteremshia Qur'an tukufu, kitabu kitukufu ambacho amesema Mwenyezi Mungu ndani yake: "Hakifikiwi na upotovu mbele yake wala nyuma yake..." [Fusswilat: 42].
Na alikuwa Nabii Muhammad rehema na amani zimfikie ndiye mwisho wa Mitume na Manabii, kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "...bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii..." [Al-Ahzab: 40].
Kuzaliwa kwake na kukua kwake:
Alizaliwa Mtume Muhammad -Sala na amani ziwe juu yake- Makkah mwaka 570 Miladia. Alifishwa baba yake kabla ya kuzaliwa kwake, na akafishwa mama yake akiwa mdogo, akalelewa na babu yake Abdulmuttwalib, kisha baba yake mdogo Abuu Twaalib ambaye alimlea vizuri, alifanya kazi katika ujana wake akiwa mchungaji wa kondoo, na zilionekana kwake alama za uungwana na uanaume wa mapema, alikuwa akimuabudu Mwenyezi Mungu katika mila ya Ibrahim, akiwa mbali na ushirikina na mambo ya masanamu.
Mwanzo wa Utume:
Alikuwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, akijitenga peke yake katika pango la Hiraa katika mji wa Makkah, akitafakari na kumuabudu Mwenyezi Mungu, mpaka akamjia Malaika Jibrili, amani iwe juu yake, na wahyi (ufunuo), na kuanzia siku hiyo ulianza ujumbe wa nuru uliodumu kwa miaka ishirini na tatu.
Kulingania huko Makka:
Alianza Nabii Muhammad -rehema na amani ziwe juu yake- ulinganizi wake kwenye Uislamu kwa siri, kisha akaitangaza baina ya watu wake, na hawakumuitikia, na pamoja na hayo aliendelea katika kufikisha uislamu kwa hekima na subira.
Walimuamini yeye wanaume na wanawake kutoka Makka, kisha likamwitikia wito wake kundi miongoni mwa watu wa mji ulio karibu na Makka ukiitwa Yathriba, mji ambao sasa jina lake limekuwa Madina Munawwara, basi Waislamu wakaanza kuhamia huko kwa amri kutoka kwake.
Kuhama na kujenga Jamii ya Kiislamu:
Alihamia Mtume Muhammad -rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- katika mji wa Madina Munawwara, na huko akaasisi jamii iliyosimama juu ya uadilifu, na udugu, na imani, na ushirikiano, na yakaenea mafundisho ya Uislamu, na wakaanza watu kuingia humo makundi kwa makundi kwa kuridhia na yakini.
Na baadhi ya makabila yalijaribu kuupiga vita Uislamu, lakini Mwenyezi Mungu alimnusuru Nabii wake, na Waislamu wakaweza kuzilinda nafsi zao na kudhihirisha haki.
Tabia za Mtume kabla ya Utume:
Alijulikana Mtume -rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- kuanzia utotoni mwake kwa tabia njema za juu, ambazo Mwenyezi Mungu alizisifia kwa kauli yake katika Qur'ani: "Na hakika wewe una tabia tukufu." [Al Qalam: 4].
Alikuwa mkweli hasemi uongo, na muaminifu anahifadhi haki, mkarimu anawafanyia wema mafakiri, mwenye kujishusha anakaa na wanyonge, mvumilivu mpole harudishi ubaya kwa mfano wake.
Na watu wa Makkah walikuwa wakiweka amana zao kwake, hata wale waliokuwa wakimfanyia uadui, kwa kumuamini kwamba yeye hafanyi khiyana.
Tabia za Mtume baada ya Utume:
Tabia zake zilizidi ukamilifu baada ya kuwa Nabii, na alikuwa Mtume Muhammadi -rehema na amani ziwe juu yake- ni rehema kwa walimwengu, kama alivyomsifu Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Nasi hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu wote." [Al-Anbiya: 107].
Na alikuwa mwenye kutabasamu daima, mzuri wa maingiliano, mlaini wa kauli, na mwenye kutimiza ahadi zake.
Amesema Nabii Muhammad rehema na amani ziwe juu yake kuhusu ujumbe wake: "Hakika bila shaka nimetumwa ili nitimilize tabia njema." [Imepokelewa na Ahmad].
Na wakati wa kurudi kwake Makka, aliwasamehe maadui zake pamoja na kuwa na uwezo juu yao, na akaonyesha ujasiri mkubwa katika hali ngumu, na alikuwa muadilifu kuliko watu wote.
Na ukweli ulikuwa msingi wa maisha yake, wala hakujulikana kwa uongo kamwe, na alikuwa Mtume Muhammad -rehema na amani ziwe juu yake- akiwahimiza watu kwenye ukweli kwa kauli yake: "Shikamaneni na ukweli, kwani ukweli hupelekea katika wema." [Imepokelewa na Bukhari].
Ama uaminifu ulikuwa ni tabia iliyothabiti kwake; basi yeye alikuwa ni muaminifu katika kufikisha wahyi, muaminifu katika kuhukumu baina ya watu, na muaminifu katika kila jambo miongoni mwa mambo ya maisha yake.
Na alisema Mtume Muhammad rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Hana imani asiyekuwa na uaminifu." [Musnad Abii Daud].
Ujumbe wa msingi wa Mtume -rehema na amani ziwe juu yake-:
Mtume -rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- aliwalingania watu katika kumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na kuacha kuabudu chochote kinyume na Yeye, na huu ndio ulinganizi wa manabii wote waliotumwa kabla yake, na aliwafundisha watu namna ya kumuabudu Mwenyezi Mungu ibada iliyo sahihi, na akawatahadharisha na shirki, na kumsemea Mwenyezi Mungu bila ya elimu, na hii ndiyo misingi ya ulinganizi wake.
Kufariki kwa Mtume Muhammad -rehema na amani ziwe juu yake-:
Baada ya Mwenyezi Mungu kuitimiza dini kupitia kwake, na watu wengi kuingia katika dini hiyo, alipatwa Nabii Muhammad -rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- na homa kali, na alifishwa siku ya juma tatu inayoafikiana na tarehe 8 Juni, mwaka wa 632 miladia, akiwa na umri wa miaka sitini na tatu, na akazikwa katika mji wa Madina Munawwara.
Somo la Kumi na Mbili:
Kufundisha Suratul Kauthar na Suratun Nasri
Suratul Kauthar:
"1. Hakika tumekupa Al-Kawthar (heri nyingi). 2. Basi swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako Mlezi. 3 Hakika anayekuchukia ndiye aliye mpungufu mno." [Al-Kauthar: 1-3]
Kufundisha kwa sauti.
Suratun Nasri:
"1. Itakapokuja nusura ya Mwenyezi Mungu na ushindi. 2. Na ukaona watu wanaingia katika Dini ya Mwenyezi Mungu kwa makundi. 3. Basi zitakase sifa za Mola wako Mlezi, na umwombe msamaha. Hakika Yeye ndiye anayepokea toba mno." [An Nasri: 1-3]
Kufundisha kwa sauti.
Somo la Kumi na Tatu:
Dharura Tano
Dharura tano:
Ni mambo ya msingi ambayo kila mtu anayategemea ili aishi maisha mema na yenye heshima. Nayo ni: Dini, Nafsi, Akili, Kizazi, na Mali.
Na kuhifadhi maslaha haya kunakuwa kwa mambo mawili:
(1) Kuisimamisha.
(2) Kuichunga na kuihifadhi kutokana na upuuzi na kasoro.
Madhambi makubwa katika Uislamu:
Madhambi makubwa ni yale madhambi makubwa na yaliyoharamishwa ambayo Mwenyezi Mungu na Mtume wake Muhammad -rehema na amani ziwe juu yake- wametahadharisha nayo tahadhari kali, na katika madhambi makubwa katika Uislamu:
1- Kumshirikisha Mwenyezi Mungu:
Uislamu ulikuja kuhifadhi dini ya mwanadamu, na kwa hivyo umeharamisha shirki; kwa sababu yenyewe ni hatari kubwa kwa imani na mwanadamu.
Kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Hakika, Mwenyezi Mungu hafuti dhambi ya kushirikishwa, na hufuta dhambi ya yale yasiyokuwa hayo kwa amtakaye. Na mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, basi hakika amezua dhambi kubwa." [An-Nisaa :48]
2- Kuua nafsi:
Uislamu umekuja kuhifadhi nafsi ya mwanadamu, na kwa hivyo umeharamisha kuuwa mtu.
Kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Wala msiiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu aliiharamisha isipokuwa kwa haki." [Al An'am: 151].
3- Zinaa:
Uislamu umekuja kuhifadhi nasaba na heshima, na kwa hivyo basi umeharamisha kuanzisha mahusiano nje ya ndoa ya kisheria.
Kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya." [Al-Israa: 32].
4. Kunywa pombe na vilevi:
Uislamu umekuja kuhifadhi akili, na kwa ajili hiyo ukaharamisha kila kinacholevya na kuharibu akili.
Kama alivyosema Mtume Muhammad -rehema na amani ziwe juu yake-: "Kila kilevi ni pombe, na kila kilevi ni haramu." [Hadithi hii wamekubaliana juu ya usahihi wake Bukhari na Muslim].
5- Wizi na kula mali za watu kwa dhuluma:
Uislamu umekuja kuhifadhi mali, na kwa hivyo umeharamisha kuchukua mali za watu bila ya haki. Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Wala msiliane mali zenu kwa batili..." [Al-Baqarah: 188].
Na hilo linajumuisha ghushi, rushwa, wizi, na mengineyo.
Somo la Kumi na Nne:
Hukumu ya baadhi ya vyakula katika Uislamu
Uislamu ni dini kamili inayomuongoza Muislamu katika mambo yote ya maisha yake, hata katika chakula chake na kinywaji chake.
Muislamu hali kwa ajili tu ya kushiba, bali ili aupe nguvu mwili wake katika kumtii Mwenyezi Mungu, na aishi maisha mazuri, na amshukuru Mola wake Mlezi kwa neema zake.
Vyakula halali (vizuri):
Katika Uislamu, kila ambacho haikuja dalili ya uharamu wake kama mimea, matunda na nafaka, basi hicho ni halali.
Kama ambavyo wanyama na ndege wanaoruhusiwa, kama vile: ngamia, ng'ombe, kondoo, kuku na sungura ni halali kuliwa, kwa sharti wachinjwe uchinjaji sahihi wa Kiislamu, pamoja na kutaja jina la Mwenyezi Mungu wakati wa kuchinja.
Kama alivyosema Mwenyezi Mungu ndani ya Qur'ani tukufu: "Enyi watu! Kuleni vilivyo katika ardhi, halali na vizuri..." [Al-Baqarah: 168].
Na mawindo yote ya baharini ni halali, sawa yakiwa hai au yamepatikana yamekufa.
Vyakula vilivyo haramu:
1- Mzoga:
Yaani: Mnyama aliyekufa bila kuchinjwa kisheria.
Mfano: Ng'ombe aliyekufa mwenyewe au aliyenyongwa, isipokuwa ikiwa Muislamu atamdiriki akiwa hai na kumchinja kabla ya kufa kwake, basi hapo atakuwa halali.
2- Damu iliyomwagika:
Nayo ni damu ya kumiminika ambayo hutoka wakati wa kuchinja.
Ama damu inayobaki katika nyama au ini, basi si haramu.
3- Nyama ya nguruwe:
Na ni haramu kwa sehemu zake zote na bidhaa zake (hata mafuta na ngozi).
4- Kilichochinjwa kwa ajili ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu au kilichotajiwa jina lisilokuwa jina la Mwenyezi Mungu wakati wa kuchinjwa kwake:
Na hivyo ni kwamba ni wajibu kwako wakati wa kuchinja mnyama kutaja jina la Mwenyezi Mungu juu yake, amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Basi kuleni katika vile vilivyotajiwa jina la Mwenyezi Mungu, ikiwa mnaziamini Aya zake." [Al-An'am: 118].
Mfano: Kuchinja kwa ajili ya masanamu, au mawalii, au kiumbe yeyote asiyekuwa Mwenyezi Mungu kama njia ya kujiweka karibu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Hakika Yeye amekuharamishieni mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilichotajiwa, katika kuchinjwa kwake, jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Lakini aliyefikiwa na dharura bila ya kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu." [Al-Baqarah: 173].
Baadhi ya wanyama walio haramu:
Kile ambacho Mweka Sharia ameamrisha kukiua, basi hicho ni haramu:
Mfano: Mjusi, panya, nyoka na nge.
Na kila chenye meno yaliyochongoka katika wanyama wanaoshambulia:
Kwa sababu Mtume Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake "Alikataza kula kila chenye meno yaliyochongoka katika wanyama wanaoshambulia." [Imepokelewa na Bukhari na Muslim].
Yaani: kila mnyama anayewashambulia na kuwala wenzake anayetumia meno yake katika kuwinda na kuua, kama vile:
Simba - Mbwa mwitu - Mbwa - Chui - Dubu - Paka - Nyani.
Na kila chenye kucha kali (za kuwindia) katika ndege:
Kwa sababu Mtume Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake "Alikataza kula kila chenye kucha kali (za kuwindia) katika ndege." [Imepokelewa na Bukhari na Muslim].
Yaani: Ndege wawindaji wenye kuwinda kwa kucha zao, kama vile:
Kozi - Tai - Kipanga - Furukombe.
Vilevi na Madawa ya Kulevya:
Nayo ni kila kinachoondoa akili kama vile pombe, bangi, afyuni... n.k.
Kama alivyosema Mtume Muhammad -rehema na amani ziwe juu yake-: "Kila kilevi ni haramu." [Hadithi hii wamekubaliana juu ya usahihi wake Bukhari na Muslim].
Na kwa kuwa inadhuru mwili, akili, dini na mengineyo, na kila kinacholeta madhara ya hakika au yenye uwezekano mkubwa ni haramu katika Uislamu.
Hekima ya hukumu za chakula:
Uislamu unamtakia Muislamu aishi maisha mazuri, yenye afya na safi.
Basi chakula cha halali kizuri husafisha mwili, na hutakasa moyo, na huifanya dua kujibiwa.
Ama chakula haramu kinaharibu moyo, na kinazuia baraka; kwa sababu ni miongoni mwa vichafu. Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "...anawaharamishia viovu..." [Al A'raf: 157].
Na alisema Mtume Muhammad rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Hakika Mwenyezi Mungu ni mzuri hakubali ila vizuri." [Imepokelewa na Muslim].
Somo la Kumi na Tano:
Cheo cha Mwanamke katika Uislamu
Uislamu umekuja ukiwa ni rehema kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa walimwengu, na ukamuokoa mwanamke kutokana na dhuluma, na kumnyanyua katika cheo chake halisi.
Basi yeye katika Uislamu ni mwanadamu aliyekirimiwa, ana haki zake kama ambavyo mwanaume ana haki zake, na Mtume Muhammad -rehema na amani ziwe juu yake- amewausia wanaume kuwatendea wema wanawake, akasema: "Watendeeni wanawake wema." [Imepokelewa na Muslim].
Na Uislamu umempa mwanamke haki yake katika mirathi baada ya kwamba alikuwa akinyimwa, na umemuwajibishia mume kutoa matumizi kwake hata kama akiwa tajiri.
Kama alivyompa haki ya kuchagua mwenza, na wala hakuna yeyote anayemlazimisha kuolewa na asiyemtaka.
Na katika Uislamu mwanamke anaweza kufanya kazi katika yale yanayoendana na maumbile yake, na kushiriki katika kuitumikia jamii yake, kama walivyofanya Maswahaba wanawake katika zama za Nabii Muhammad, rehema na amani zimshukie.
Basi alikuwa Swahabiyyat Rufaidah Al-Aslamiyyah akiwatibu majeruhi, na Swahabiyyat Zainab bint Jah'shi akifanya kazi kwa mikono yake na kutoa katika njia ya Allah, na wanawake wengineo wengi.
Na Uislamu umemtukuza mama:
Kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema..." [Al Israai: 23].
Na amemkirimu binti na Dada:
Kama alivyosema Mtume Muhammad -rehema na amani ziwe juu yake-: "Atakayekuwa na dada wawili au mabinti wawili, akawatendea wema muda wote walio naye, mimi nitakuwa na yeye Peponi." [Musnad Abii Daud].
Na miongoni mwa heshima kubwa zaidi ya Uislamu kwake ni Stara:
Uislamu haukutosheka tu na kumpa haki zake, bali umehami heshima yake ili asiwe bidhaa yenye kuwekwa wazi kwa kutazamwa, na ukamwekea sheria ya vazi lenye kuhami heshima yake na kumlinda kutokana na kushushwa thamani, wala si kwa ajili ya kumdhalilisha.
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Ewe Nabii, waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana kwa hivyo wasiudhiwe.." [Al-Ahzab: 59].
Amemuwajibishia Mwenyezi Mungu mwanamke wa Kiislamu kuvaa hijabu kwa wanaume wa kando, na hilo ni kwa kuvaa vazi la heshima, lenye kusitiri, pana, lisiloonesha ndani wala kutiwa manukato, na lisilokuwa na mapambo yanayovutia, na wala halifanani na vazi la wanaume. Na mwanamume wa kando ni yule ambaye si mume wa mwanamke wala miongoni mwa maharimu wake [2]. [2] Maharimu wa mwanamke ni mwanamume ambaye haijuzu kwake kisheria kumuoa kwa uharamu wa milele kwa sababu ya ukaribu wa kiukoo, au kunyonya, au ukwe, na maharimu wanajumuisha asili (baba na mababu), matawi (watoto na wajukuu zao), ndugu wa kiume, baba wadogo na wakubwa, wajomba, watoto wa kiume wa ndugu wa kiume na dada, pamoja na mume wa mama (baada ya kumwingilia), na baba mkwe, na mtoto wa kiume wa mume.
Somo la Kumi na Sita:
Ndoa katika Uislamu
Ndoa katika Uislamu inalenga kujenga familia thabiti na njema.
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Na katika Ishara zake ni kuwa aliwaumbia wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye ameweka mapenzi na rehema baina yenu..." Ar-Ruum: 21
Na hakika Mwenyezi Mungu ameweka sheria ya ndoa, na amebainisha kwamba hii ndiyo hali ya Mitume na Manabii; ili watu wafuate mfano wao.
Alisema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Na hakika Sisi tulikwishawatuma Mitume kabla yako, na tukawafanya wawe na wake na watoto..." [Ar-Ra'd: 38].
Na miongoni mwa malengo makuu ya ndoa:
Kudumisha aina ya binadamu, na kusalimika kwa jamii na kuilinda kutokana na kuporomoka kwa maadili, na kutimiza maumbile ya kibinadamu na kutosheleza matamanio kwa njia sahihi, na kuhifadhi kizazi, na kuanzisha familia njema.
Na miongoni mwa ukamilifu wa hekima: ni kwamba Mwenyezi Mungu amehalalisha katika Uislamu talaka baina ya wanandoa, na wala haikimbiliwi isipokuwa wakati wa dharura, na baada ya kumaliza njia za kutafuta suluhu baina yao, kwa mujibu wa hukumu maalumu.
Mambo yaliyo wajibu kwa wanandoa:
Uislamu haukuacha jambo la ndoa bila ya vidhibiti vyenye kuhukumu mafungamano kati ya wanandoa na kuyaweka wazi, hakika Uislamu umeweka wajibu na haki juu ya kila upande; ili maisha ya ndoa yanyooke kwayo, na mapenzi yadumu kwayo, na miongoni mwa wajibu huu muhimu zaidi ni:
Wajibu wa mume:
As-swadaaq (Mahari), nayo ni mali anayoilipa mume kwa mwanamke ikiwa ni badala ya mkataba wa nikaha, na hiyo si thamani ya kifedha kwa ajili ya kummiliki mke, bali ni haki ya kimali aliyomwekea Mwenyezi Mungu kisheria. Na Mwenyezi Mungu amewaamrisha wanaume kuamiliana na wanawake kwa wema na kuwathamini, na kuwa na tabia njema kwao, na kuwakirimu na kuhifadhi siri zao, na akatahadharisha dhidi ya kuwadhalilisha na kuwapuuza, na akatoa onyo kali kwa anayewadhulumu, na akahimiza kuzingatia maumbile yake, na kutimiza haki yake ya kiasili na kimaumbile, na kutoa matumizi juu yake kwa wema katika chakula, mavazi na makazi, kila mmoja kulingana na uwezo wake na hali yake ya kimali.
Somo la Kumi na Saba:
Tabia na adabu za kisheria
Uislamu ni dini iliyokusanya vitu vyote ambayo haikomei katika ibada, bali ni mfumo wa maisha wenye kukamilika unaopangilia uhusiano wa mwanadamu na Mola wake na watu, bali hata na ulimwengu unaomzunguka. Na tabia na adabu za kisheria zinahesabika kuwa ni katika nguzo muhimu zaidi za mfumo huu, kwani zinalenga kumjenga mtu mwema, na jamii inayotawaliwa na upendo, uadilifu na huruma.
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani, na kuwapa jamaa, na anakataza uchafu, na uovu, na dhuluma..." [An-Nahl: 90].
Maana ya Tabia na Adabu (Heshima):
Tabia: Ni sifa thabiti katika nafsi, zinazoelekeza mienendo ya mwanadamu kwenye kheri, kama vile: ukweli, uaminifu, na uadilifu. Nazo ndizo zinazomfanya Muislamu apendwe kwa Mwenyezi Mungu na kwa watu.
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Waambie waja wangu waseme maneno mazuri mno..." [Al-Israa: 53].
Adabu: Tabia njema ambazo Muislamu anazitekeleza katika maisha yake ya kila siku, kama vile: adabu za kuzungumza, kula, na muamala.
Umuhimu wa nafasi ya tabia na adabu katika Uislamu:
Kuwa ni miongoni mwa makusudio muhimu zaidi ya kutumwa kwa Mtume Muhammad rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake kwa watu:
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Yeye ndiye aliyemtuma Mtume kwa watu wasiojua kusoma na kuandika, awasomee Aya zake na awatakase..." [Al-Jumu'a: 2], Na miongoni mwa neema za Mwenyezi Mungu kwa Waumini ni kumtuma Mtume wake ili kuwafundisha Qur'ani na kuwatakasa, na maana ya kutakasa ni: kutakasa moyo kutokana na ushirikina na tabia mbaya; kama vile chuki, na husuda, na desturi mbaya.
Na alisema Mtume Muhammad rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Kwa hakika nimetumwa ili kutimiliza tabia njema." [Imepokelewa na Ahmad]
Ukamilifu wa imani:
Tabia ni sehemu ya imani. Amesema Mtume Muhammad rehema na amani zimfikie: "Muumini aliyekamilika kiimani ni yule mwenye tabia njema zaidi kuliko wengine." [Imepokelewa na Tirmidhi, Abuu Daud na Ahmad].
Kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake:
Na amesema rehema na amani ziwe juu yake: "Hakika katika watu wanaopendeka zaidi kati yenu kwangu mimi, na atakayekaa karibu zaidi kati yenu na mimi siku ya Kiyama ni yule atakayekuwa na tabia njema zaidi kati yenu." [Imepokelewa na Tirmidhi].
Mifano ya tabia:
● Ukweli: Ni mwanadamu kusema haki na kuitendea kazi. Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kuweni pamoja na wakweli." [At-Tauba: 119].
●Amana: Kutekeleza haki kwa wenyewe, na kutofanya khiana. Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Hakika Mwenyezi Mungu anawaamrisha kwamba mzirudishe amana kwa wenyewe..." [An Nisaai: 58].
●Rehema: Upole, na kumhurumia mdogo na mkubwa.
● Uadilifu: Kumpa kila mwenye haki haki yake, hata kwa yule tunayetofautiana naye.
● Unyenyekevu: Kutokujikweza kwa watu, na kuwatendea kwa upole.
● Subira: Kuwa imara katika utiifu na kuvumilia matatizo kwa kuridhia. Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Na wabashirie wanaosubiri." [Al-Baqara: 155].
●Haya: Ni Muislamu kuona haya kufanya yanayomkasirisha Mwenyezi Mungu, au kuwafanyia ubaya watu.
Mifano ya adabu:
❖Adabu za kuzungumza:
Kuzungumza ukweli, kushusha sauti, kutowakatiza wengine, kuchagua maneno mazuri, kujiepusha na matamshi mabaya.
❖Adabu za salamu:
Kuanza kwa maamkizi, na kuyaitikia kwa yaliyo mazuri zaidi yake, na iwe kwa sauti iliyo wazi pamoja na tabasamu. Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Na mnapoamkiwa kwa maamkizi yoyote, basi itikieni kwa yaliyo mazuri zaidi kuliko hayo, au yarejesheni hayo hayo..." [An nisaai: 86]
Adabu za kula katika Uislamu:
Kula katika Uislamu si ada tu, bali ni ibada na shukurani kwa Mwenyezi Mungu juu ya neema zake, na ametufundisha Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- adabu zinazofanya chakula kuwa sababu ya baraka, afya na upendo baina ya watu, miongoni mwazo ni:
● Muislamu anuie kwa kula kwake apate nguvu ya kufanya kheri na kumtii Mwenyezi Mungu.
● Kusema: "Bismillah (kwa jina la Mwenyezi Mungu)" kabla ya kuanza, basi ikiwa atasahau aseme atakapokumbuka: "Bismillahi fii awwalihi wa aakhirihi (Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwanzo wake na mwisho wake)."
● Kula kwa mkono wa kulia.
● Kula kile kinachomuelekea mtu katika sahani ya pamoja, na kutonyoosha mkono kwenye kile kilicho mbele ya wengine.
● Kumshukuru Mwenyezi Mungu baada ya kumaliza.
●Kuhifadhi chakula kilichozidi na kukiheshimu.
Kuishi pamoja katika Uislamu:
Uislamu ni dini ya huruma na uadilifu, na kimsingi unalingania kwenye amani na kushirikiana katika heri baina ya watu wote, hata kama zimetofautiana dini zao au koo zao au lugha zao, kwani Mwenyezi Mungu amewaumba wanadamu wakiwa tofauti tofauti kwa hekima kubwa. Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Enyi watu! Hakika Sisi tumewaumba kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mcha Mungu zaidi katika nyinyi." [Al Hujrati: 13].
Basi Uislamu haulinganii katika kujitenga au chuki, bali katika kujuana na kushirikiana katika kheri, na kuheshimiana, na muamala mzuri.
Na kwa hakika alikuwa Mtume Muhammad -rehema na amani ziwe juu yake- ni mfano katika uzuri wa kuishi pamoja; kwani alikuwa akimtembelea jirani yake myahudi akiumwa, na akikubali mialiko ya wasiokuwa waislamu, na akiamiliana nao kwa uadilifu na huruma, na akihimiza kuunga udugu hata kama walikuwa wanatofautiana na huyo mwenye kuunga katika dini yake. Amesema Mtume Muhammad -rehema na amani ziwe juu yake-: "Muumini ni yule ambaye watu wanamuamini juu ya damu zao na mali zao."" [Imepokelewa na Ahmad na At-Tirmidhi].
Basi Muislamu hadhulumu mtu yeyote, na wala hamfanyii ubaya yule anayetofautiana naye, bali anakuwa mwenye huruma, mwenye kupenda kheri, anaamiliana vizuri na wote; kwa sababu tabia njema ni lugha wanayoielewa binadamu wote.
Kuwatendea wema wazazi wawili
Miongoni mwa maadili makubwa ambayo Uislamu umeyatilia mkazo ni kuwatendea wema wazazi wawili, yaani kuwafanyia wema, na kuwahudumia, na kuwaombea dua, na kutowapandishia sauti. Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema..." [Al Israai: 23]
Na kuwatendea wema wazazi wawili hakukomei kwa waislamu miongoni mwao tu, bali huwajumuisha wasio waislamu pia, kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Na pindi wakikulazimisha kunishirikisha na ambayo huna elimu nayo, basi usiwatii. Lakini kaa nao kwa wema duniani..." [Luqman: 15].
Haki ya jirani
Kama ambavyo Uislamu umeusia juu ya jirani, sawa atakuwa Muislamu au asiyekuwa Muislamu.
Na alisema Mtume Muhammad rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Hakuacha Jibril kuendelea kuniusia kuhusu jirani, mpaka nikadhania kwamba yeye atamrithisha." [Hadithi hii wamekubaliana juu yake Bukhari na Muslim].
Na miongoni mwa namna za kumfanyia wema jirani:
● Kumtolea salamu na kumuuliza hali yake.
● Kumsaidia wakati wa uhitaji.
● Kuzuia maudhi kwake, na kutonyanyua sauti au kumsumbua.
● Kushiriki katika furaha, na kutoa msaada katika shida.
Amesema Mtume Muhammad rehema na amani ziwe juu yake: "Mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, basi na amkirimu jirani yake." [Hadithi hii wamekubaliana juu yake Bukhari na Muslim].
Basi Muislamu anadhihirisha tabia zake njema nyumbani kwake na kwa majirani zake, hivyo anakuwa mpendwa miongoni mwao, kiigizo chema katika kuamiliana, na chanzo cha usalama na amani.
Somo la Kumi na Nane:
Dua na Dhikiri
Ya kwanza: Maana ya Dua na umuhimu wake:
Dua imewekwa kisheria katika nyakati zote na hali zote, kwa mfano pindi mwanadamu anapohisi dhiki au huzuni, basi mlango wa kwanza anaoukimbilia ni mlango wa Mwenyezi Mungu, naye yuko karibu nasi kuliko kitu kingine chochote, na hakika Mwenyezi Mungu alimfundisha Nabii wake -rehema na amani ziwe juu yake- katika Qur'ani pindi watu walipomuuliza kuhusu Mola wao kuwa Yeye yuko karibu nao, na kwamba wakimuomba kwa ukweli atawajibu.
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Na waja wangu watakapokuuliza kunihusu Mimi, basi Mimi kwa hakika nipo karibu. Ninaitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka." [Al-Baqarah: 186].
Na miongoni mwa dua alizofundisha Mtume Muhammad rehema na amani ziwe juu yake wakati wa msongo wa mawazo na huzuni ni kauli: "Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mpole, hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa Arshi takatifu, hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na Mola Mlezi wa Arshi tukufu." [Hadithi hii wamekubaliana juu yake Bukhari na Muslim]. Dua hii inaleta utulivu, na inamkumbusha mja ukaribu wa Mwenyezi Mungu na rehema zake.
Pili: Maana ya Dhikri:
Dhikiri ni kumkumbuka Mwenyezi Mungu kwa moyo na ulimi.
Nalo ni jambo kubwa zaidi linalohuisha moyo, na kuimarisha imani.
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Eleweni vyema! Kwa kumtaja Mwenyezi Mungu ndiyo nyoyo hutua! [Ar-Ra'd: 28].
Kwa nini dhikiri ni muhimu?
❖Dhikri ni sifa miongoni mwa sifa za Waumini:
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "...na wanaume wanaomdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi na wanawake wanaomdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi, Mwenyezi Mungu amewaandalia msamaha na ujira mkubwa." [Al-Ahzab: 35].
❖ Dhikri ni uhai wa moyo:
Amesema Mtume Muhammad rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Mfano wa yule anayemtaja Mola wake, na yule asiyemtaja Mola wake, ni mfano wa aliye hai na aliyekufa." [Hadithi hii wamekubaliana juu yake Bukhari na Muslim].
❖ Kumtaja Mwenyezi Mungu hukukinga kutokana na Shetani:
Mtume Muhammad -rehema na amani ziwe juu yake- aliifananisha dhikri na mtu mmoja anayekimbia kutoka kwa maadui zake kuelekea kwenye ngome imara inayomlinda.
Basi vivyo hivyo kumtaja Mwenyezi Mungu humkinga Muislamu kutokana na Shetani.
❖ Kumtaja Mwenyezi Mungu hupunguza mahangaiko ya dunia:
Kila moyo unavyojaa kwa kumtaja Mwenyezi Mungu, wasiwasi wa dunia huwa mdogo machoni pake, na huimarika subira yake na nguvu yake.
❖ Dhikri inafungua mlango wa uhusiano wa kudumu na Mwenyezi Mungu:
Atakayemtaja Mwenyezi Mungu daima anahisi ukaribu wake, na anapata utulivu na faraja.
Adhkari nyepesi na zenye malipo makubwa:
Kusoma Qur'ani ni dhikri bora zaidi, kwa kila herufi kuna mema 10. Amesema Mtume -rehema na amani ziwe juu yake-: "Atakayesoma herufi moja katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, basi atapata jema moja kwa herufi hiyo, na jema hilo hulipwa mara kumi mfano wake." [Imepokelewa na Tirmidhi]. Na amesema Mtume Muhammad rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Someni Qur'ani; kwani, itakuja Siku ya Kiyama kama muombezi kwa wenye kuisoma." [Imepokelewa na Muslim].
Na kusoma Qur'ani huhifadhi imani na huimarisha uhusiano na Mwenyezi Mungu.
Hizi ni baadhi ya Adhkari (Dua) ambazo ni vyema kwa Muislamu kuzikariri:
●Utakasifu ni wa Mwenyezi Mungu, na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu.
● Laa ilaaha illa llah, wa Allaahu Akbaru. Yaani: Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mkubwa.
● Hakuna uwezo wala nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu.
●Ninamuomba msamaha Mwenyezi Mungu.
● Utakasifu ni wa Mwenyezi Mungu na sifa ni zake.
● Utakasifu ni wa Mwenyezi Mungu Mkuu.
●Hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake asiye na mshirika, Mwenye ufalme na Mwenye sifa na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza.
Somo la Kumi na Tisa:
Fadhila za kulingania na kuelekeza kwa Mwenyezi Mungu
Kulingania kwa Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa matendo makubwa katika Uislamu, nako ni kwa Muislamu kuwaelekeza watu kwenye kheri, na kuwafahamisha kuhusu Mwenyezi Mungu, na Uislamu, na tabia njema.
Amesema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Na ni nani mbora zaidi wa kusema kuliko aitaye kwa Mwenyezi Mungu na akatenda mema, na akasema: Hakika mimi ni katika Waislamu?" [Fuswilat: 33].
Yaani: Hakuna kauli wala kitendo kizuri na bora zaidi kuliko kulingania kwa Mwenyezi Mungu, pamoja na matendo mema.
Na ametoa habari Mtume rehema na amani ziwe juu yake kwamba kuongoka kwa mtu mmoja katika Uislamu kwa sababu yako ni bora kuliko utajiri mkubwa zaidi wa dunia ambao watu wanaupenda, na kwamba malipo ya uongofu huu utayakuta Siku ya Kiyama yakiwa makubwa sana.
Muislamu mpya anazo:
● Ujira wa mema aliyoyafanya kabla ya kusilimu anaposilimu na kuufanya Uislamu wake kuwa mzuri. Na hakika Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- alimbashiria mtu mmoja alipokuja kusilimu: kuwa matendo mema aliyokuwa akiyafanya kabla ya kusilimu; miongoni mwa sadaka yake, na kuwasaidia wengine, Mwenyezi Mungu atambakishia hayo, na atamlipa ujira kwayo.
● Ujira wa Uislamu wake na uthabiti wake.
● Malipo ya yule anayeongoka kwa sababu yake. Amesema Mtume, rehema na amani zimshukie: "Atakayelingania katika uongofu, atakuwa kwake kapata malipo mfano wa malipo ya aliyemfuata, halipunguzi hilo chochote katika malipo yao." [Imepokelewa na Muslim].
Kudhihirisha Uislamu:
Ikiwa Muislamu mpya atahofia juu ya nafsi yake madhara makubwa au hatari ya kweli, inajuzu kwake kuficha Uislamu wake, mpaka awe salama.
Ikiwa hakuna hofu ya kweli, basi ni bora kudhihirisha Uislamu kwa utulivu na hekima.
Kubadilisha jina:
Si wajibu kubadilisha jina baada ya Uislamu, isipokuwa ikiwa lina maana iliyoharamishwa, kama:
● Jina lenye utumwa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu.
●Jina lenye maana mbaya.
Ikiwa jina ni la kawaida au lina maana nzuri, basi si lazima kulibadilisha, na Uislamu haushurutishi jina la Kiarabu.
Ni vipi Muislamu ataanza kulingania?
Ufikishaji unaanza kwenye mwenendo kabla ya maneno.
Kwa nini tunawalingania watu?
Kwa sababu tunawapendea mema, na tunawahurumia, na tunawatakia uongofu na kusalimika.
Lakini tunapaswa kukumbuka kwamba uongofu uko mkononi mwa Mwenyezi Mungu, na sisi jukumu letu ni kufikisha tu.
Anza na nafsi yako: dumisha sala, jifunze dini yako, na uache haramu, na uwe na tabia njema; kwa sababu watu wanaona matendo yako kabla ya maneno yako.
Dini ni muamala: Tabia njema ni miongoni mwa njia kubwa za kulingania kwa Mwenyezi Mungu (daawa); ukweli, uaminifu, huruma, na heshima, yote haya yanaweza kuwa sababu ya uongofu wa mtu.
Mbele ya wengine wewe unawakilisha Uislamu, kwa maana kwamba vitendo vyako vinatoa taswira ya dini. Basi watu wakiona tabia njema watasema: Huu ndio Uislamu, na wakiona kinyume huenda wakasema kinyume na hivyo. Amesema Mtume rehema na amani zimfikie: "Kwa hakika nimetumwa ili kutimiliza tabia njema." [Imepokelewa na Ahmad].
Anza na wale walio karibu na wewe zaidi: watu wa familia, marafiki, wafanyakazi wenzako, kwa upole na bila ya shinikizo.
Zungumza kwa kadiri ya ujuzi wako: Jibu kwa yale unayoyajua, na ikiwa hujui basi sema: Sijui, na uelekeze katika tovuti zifuatazo.
Katika adabu za kulingania na kuelekeza:
● Kuchagua wakati unaofaa kwa mazungumzo.
● Upole na kutulia.
● Kutotukana au kudhihaki dini za wengine.
● Kutofanya mijadala kwa ukali.
● Kuvumilia juu ya majibu ya watu.
● Kuwaombea uongofu.
Muislamu hana jukumu la kuwaongoa watu, kwani uongofu uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu, lakini ni wajibu wake kufikisha dini kwa kadiri anavyoweza, na kila tabia njema au kauli njema huenda ikawa sababu ya uongofu wa mtu.
Somo la Ishirini:
Ninajifunza vipi hukumu za dini yangu?
Muislamu huwa na pupa ya kutekeleza dini yake kwa elimu na uelewa, wala si kwa ijtihadi na ujinga, na jambo hili linakuwa kwa kurejea kwa wanachuoni, na kuwauliza kuhusu yale yanayomtatiza miongoni mwa mambo ya dini yake, na inampasa afanye juhudi katika kutafuta elimu itakayomuwezesha kutekeleza yale aliyomfaradhishia Mwenyezi Mungu kwa usahihi, kisha ajiongezee katika maarifa ya kisheria kila anapopata wepesi.
Related books
All books
Muhutasari wenye faida kwa Muislamu mpya.32 lughaMuhutasari wenye faida kwa Muislamu mpya.
Muandaaji Muhammad Al-shihriy 2020-1441 Kwa Jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu Utangulizi
(Kitabu cha Adabu za kwenda katika Swala)11 lugha(Kitabu cha Adabu za kwenda katika Swala)
Mtunzi: Sheikh Al- islaam na alama miongoni mwa alama, kiongozi aliyerudisha upya elimu ya dini, Sheikh Muhammad bin Abdulwahhab Allah Mtukufu amrehemu. Wamefanya kazi ya kusahihisha na kulinganisha Nakala iliyoandikwa kwa mkono katika Maktaba ya Saudia kwa namba 269/86 na nakala nyingine nyingi zimechapishwa na masheikh wafuatao: Abdul karim bin Muhammad Al-laahim. Naasir bin Abdillahi Al- Twariim, Suud bin Muhammad Al- bashar. Kwa Jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu: (Mlango wa adabu za kwenda katika Swala) Ni Sunna kutoka kuiendea swala hali ya kuwa umejitwaharisha…
Mimi ni Muislamu31 lughaMimi ni Muislamu
Makala hii imebainisha maana ya Uislamu, na ni nani Muislamu, na vipi utakuwa Muislamu wa kweli, kama ilivyosheheni kwa kutaja uzuri wa Uislamu na baadhi ya adabu na tabia za hali ya juu, na nafasi ya mwanamke, na haki za ndugu wa karibu na jirani na jamii, inabainisha kuwa Uislamu unaamrisha na unaita watu kwenye kila jambo zuri, na haukatazi isipokuwa kila kilicho kibaya.
Hisnu Al-Muslim Kutoka Katika Nyiradi Za Kitabu Na Sunna41 lughaHisnu Al-Muslim Kutoka Katika Nyiradi Za Kitabu Na Sunna
Kitabu kinakusanya Adhkari kutoka katika Kitabu na Sunna ili iwe rahisi kuzikariri katika nyakati na hali mbalimbali, na kinajumuisha Dua (maombi) za kuamka, kutawadha, swala, safari, na mengineyo, jambo ambalo linamsaidia Muislamu kuikinga nafsi yake ili awe katika hifadhi ya Mwenyezi Mungu na uangalizi wake.