Skip to content
839 Hadithi

Ensaiklopidia ya Hadithi za Nabii

Chuja matokeo

Kadi 37 kati ya 839

Ondoa vichujio

Daraja la hadithi

Ametuhadithia Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- naye ni mkweli mwenye kukubaliwa: "Kwa hakika mmoja wenu hukusanywa umbile lake kwenye tumbo la mama yake mchana arobaini na nyusiku arobaini kisha anakuwa tone la manii kwa muda kama huo kisha anakuwa pande la damu kwa mfano wa siku hizo, kisha hutumwa Malaika na huamrishwa kufanya mambo manne; Hivyo basi ataandika riziki yake, na muda wa kufa kwake na matendo yake na ataandika kuwa ni muovu au ni mwema, kisha atampulizia roho, na kwa hakika mmoja wenu anaweza kufanya matendo ya watu wa Peponi kiasi ya kuwa haitobakia kati yake na kuingia Peponi isipokuwa usawa wa urefu wa mkono, basi kikamtangulia kitabu -Kadari- na akafanya matendo ya watu wa motoni na akaingia motoni, na kwa hakika mmoja wenu anaweza akafanya matendo miongoni mwa matendo ya watu wa motoni mpaka ikabakia kati yake na kuingia motoni kiasi cha usawa wa mkono kisha kikamtangulia kitabu -Kadari- akafanya mataendo ya watu wa peponi na akaingia peponi."
Sahihi Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wake
"Mimi ndiye bwana wa watu siku ya Kiyama, na je, mnajua ni kwa sababu gani hilo? Mwenyezi Mungu atawakusanya watu wa mwanzo na mwisho katika udongo mmoja, atawasikilizisha mwenye kunadi, na atawapa upeo wa kuona, na jua linaposogea, watu watafikwa na tabu na matatizo kiasi ambacho hawatoweza kuvumilia, watu watasema: Hivi hamuoni kilichowafikia, hivi hamtafuti wa kukuteteeni kwa Mola wenu Mlezi? Hapo watasema baadhi yao kuwaambia baadhi: Nendeni kwa Adam, watamuendea Adam amani iwe juu yake, watasema kumwambia: Wewe ndiye baba wa wanadam, Mwenyezi Mungu alikuumba kwa mkono wake, na akakupulizia katika roho yake, na akawaamrisha Malaika wakakusujudia, tutetee kwa Mola wako Mlezi, hivi huoni hali tuliyonayo, na huoni hali iliyotufika? Adam atasema: Hakika Mola wangu leo hii ameghadhibika ghadhabu ambayo hajawahi kughadhibika mfano wake, na hatoghadhibika tena baada yake mfano wake, na hakika alinikataza kuhusu mti mimi nikamuasi, leo nalia na nafsi yangu nafsi yangu, nendeni kwa mwingine, nendeni kwa Ibrahim, watamuendea Ibrahim na watasema: Ewe Ibrahim wewe ni Nabii wa Mwenyezi Mungu na mwandani wake katika wakazi wa Ardhini, tutetee kwa Mola wako, hivi kwani huoni hali tuliyonayo? Atasema: Hakika Mola wangu leo hii ameghadhibika ghadhabu ambayo hajawahi kughadhibika mfano wake, na hatoghadhibika tena baada yake mfano wake, na hakika mimi nilisema uongo mara tatu, leo ninalia na nafsi yangu nafsi yangu, nendeni kwa mwingine, nendeni kwa Issa bin Mariam, watamuendea Issa na watasema: Ewe Issa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na ni neno lake alilolipeleka kwa Mariam na ni roho kutoka kwake, na uliwasemesha watu ukiwa mtoto mchanga katika mbeleko, tutetee kwa Mola wako, hivi huoni hali tuliyonayo? Issa atasema: Hakika Mola wangu leo hii ameghadhibika ghadhabu ambayo hajawahi kughadhibika mfano wake, na hatoghadhibika tena baada yake mfano wake katu, na hatotaja dhambi, leo nalia na nafsi yangu nafsi yangu, nendeni kwa mwingine, nendeni kwa Muhammadi, watamuendea Muhammadi na watasema: Ewe Muhammadi wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na ni mwisho wa Manabii, na alikwisha kusamehe Mwenyezi Mungu madhambi yako yaliyotangulia na yajayo, tutetee sisi kwa Mola wako, hivi huoni hali tuliyonayo?, hapo nitaondoka na nitakwenda mpaka chini ya Arshi, nitaporomoka kumsujudia Mola wangu Aliyetakasika na kutukuka, kisha atanifungulia Mwenyezi Mungu katika sifa zake na himdi zake, na sehemu katika kumtukuza, kwa kiasi ambacho hajawahi kumfungulia yeyote kabla yangu, kisha patasemwa: Ewe Muhammadi nyanyua kichwa chako, omba upewe, na omba utetezi ukubaliwe, hapo nitanyanyua kichwa changu, na nitasema: Umma wangu ewe Mola wangu, Umma wangu ewe Mola wangu, Umma wangu ewe Mola wangu, patasemwa: Ewe Muhammadi waingize peponi katika Umma wako wale wasiokuwa na hesabu kwa kupitia mlango wa kulia katika milango ya pepo, nao watashirikiana na watu wengine pia kupita katika milango mingine tofauti na huo, kisha akasema: Namuapa yule ambaye nafsi yangu iko mkononi mwake, hakika masafa yaliyoko baina ya fremu mbili katika fremu za milango ya pepo ni sawa na masafa kutoka Makka kwenda Himyari (Yemen) au ni kama masafa ya kutoka Makka kwenda Basra (Iraq) (Km. 1287)".
Sahihi Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wake
"Hakita simama Kiyama mpaka jua lichomoze kutoka upande wa Magharibi, na likichomoza na wakaliona watu wote wataamini, na wakati huo: ((Mtu haitamfaa imani yake ambaye alikuwa hakuamini kabla, au imani yake haikufanya mambo ya kheri:158)) na kwa hakika kitasimama Kiyama na hali yakuwa watu wawili wametandaza nguo zao kwa ajili ya kuuza na kununua na wala hatoweza kuzikunja kutokana na uharaka wa Kiyama, na kwa hakika kitasimama Kiyama ghafla, na kwa hakika ataondoka mtu na maziwa aliyoyachukua kwenye chuchu za mnyama na wala asiwahi kuyanywa, na kitasimama Kiyama wakati anatengeneza josho la kunyweshea na wala asiwahi kunywesheleza, na kwa hakika kitasimama Kiyama na mmmoja wenu atainua tonge kupeleka mdomoni na wala asiweze kula."
Sahihi Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wake
"Hakika mmoja wenu anapokufa huonyeshwa makao yake asubuhi na jioni, akiwa katika watu wa peponi basi huonyeshwa katika watu wa peponi, na akiwa katika watu wa motoni basi huonyeshwa katika watu wa motoni, basi husemwa: Haya ndiyo makao yako mpaka atakapokufufua Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama".
Sahihi Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wake
"Mauti yataletwa yakiwa kama dume la Kondoo mwenye rangi mchanganyiko ya weusi na weupe,kisha muitaji ataita; Enyi watu wa peponi, basi watainua vichwa vyao na kuangalia, basi mwenye kuita atasema: Je mnamjua huyu? Nao watajibu: Ndiyo hayo ni Mauti, na wote kwa hakika wameyaona, kisha mwenye kuita atawaita: Enyi watu wa Motoni, basi watainua shingo zao na kuangalia, basi atawaambia na je mnamjua huyu basi watamjibu ndiyo haya ni Mauti, na wote kwa kakika wameyaona, hivyo basi yatachinjwa kisha atasema: Enyi watu wa Peponi,kaeni humo milele na hakuna kufa, na nyie watu wa motoni kaeni humo milele na hakuna kufa, kisha akasoma: "Na uwaonye siku ya majuto wakati hukumu ya kuingia peponi na motoni itakapotolewa Nao wapo kwenye kughafilika na wala hawaamini" (Surat Maryam:39)
Sahihi Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wake
"Hivi nisikuelezeni watu wa peponi? Kila mnyonge mwenye kujishusha, na lau kama angeliapia kwa Mwenyezi Mungu basi angelimuepusha (na kutopokea kiapo chake), hivi nisikuelezeni watu wa motoni? kila jeuri mkaidi mwenye kiburi".
Sahihi Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wake
"Jua litasogezwa karibu na viumbe Siku ya Kiyama mpaka liwe karibu nao umbali wa maili moja.", Sulaim bin 'Amir akasema: "Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu, sijui (kiwango) alimaanisha nini kwa "maili"? Je, ni umbali katika ardhi au ni kile kijiti kinachotumiwa kupaka wanja wa manga kwenye jicho." (Mtume) Akasema: "Kisha, watu watakuwa ndani ya jasho yao kulingana na matendo yao. Miongoni mwao, kuna ambaye litakuwa hadi kwenye vifundo viwili vya miguu yake. Na miongoni mwao, kuna ambaye litakuwa hadi kwenye magoti yake mawili. Na miongoni mwao, kuna ambaye litakuwa hadi kwenye nyonga zake mbili. Na miongoni mwao, kuna ambaye jasho (lake) litammeza kabisa."
Sahihi Imepokelewa Imamu Muslim
"Hakika, mwenye kiwango cha chini zaidi kati yenu katika Pepo ni kwamba ataambiwa: "Tamani!" Basi atatamani na atamani, na ataambiwa: "Je umeshatamani?" Atasema: "Nidyo." Ataambiwa: "Ni vyako vyote ulivyotamani, na mfano wake pamoja navyo."
Sahihi Imepokelewa Imamu Muslim