من معالم التوحيد

من معالم التوحيد

Miongoni mwa alama za Tauhidi (kumpwekesha Mwenyezi Mungu)

Language: lang_sw
Prepared by: Abdul Razzaq bin Abdul Mohsin Al-Badr
Version: 1.0
Translations 11
Bengali Spanish French Indonesian +7
Attachments 7
PDF
Audio
Video
+3

Miongoni mwa alama za Tauhidi (kumpwekesha Mwenyezi Mungu)

Abdul Razzaq bin Abdul Mohsin Al-Badr

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote, na mwisho mwema ni wa wachamungu. Na ninashuhudia kwamba hakuna mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu peke yake, asiye na mshirika, na ninashuhudia kwamba Muhammad ni mja wake na Mtume wake. Rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na jamaa zake na Maswahaba wake. Ama baada ya hayo:

Hakika, Tauhidi ndiyo mwanzo na mwisho wa Dini, na ndiyo ndani yake na nje yake. Nayo ndiyo (Daa'wa) wito wa kwanza na wa mwisho wa Mitume. Nayo ndiyo maana ya kusema: “Hakuna Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu.” Viumbe vyote viliumbwa kwa ajili yake, na wakatumwa Mitume, na vikateremshwa Vitabu. Na kwa ajili yake, watu waligawanyika makundi kukawa kuna Waumini na makafiri, na watu wenye furaha ni watu wa Peponi na watu waovu ni watu wa Motoni. Nao ndiyo wajibu wa kwanza juu ya mtu aliyewajibishwa kisheria, na ndiyo uhalisia wa dini ya Kiislamu, ambayo Mwenyezi Mungu hatakubali dini nyingine kutoka kwa yeyote isipokuwa hiyo. Kwa hivyo, jambo lake ni kubwa mno, na ni muhimu sana, na kila mmoja wetu anahitaji kukumbushwa na kufahamishwa juu yake. Katika makala hii, “Miongoni mwa alama za Tauhidi” kuna ufafanuzi fulani wa miangaza na alama za Tauhidi, kupitia masuala yafuatayo:

Suala la kwanza: Sifa maalumu za Tauhidi na fadhila zake

Suala la pili: Ufafanuzi wa Tauhidi na uhakika wake

Suala la tatu: Kutekeleza Tauhidi na kuikamilisha

Suala la nne: Mambo yanayobatilisha Tauhidi na kuipunguza

Suala la tano: Chanzo na chimbuko la Tauhidi

Suala la sita: Matunda ya Tauhidi na faida zake

Haya ndiyo masuala sita ambayo mazungumzo yetu yatakuwa juu yake katika makala hii kwa ufupi na kwa muhutasari. Kila moja ya masuala haya linahitaji ufafanuzi wa kina na mpana, lakini nitafupisha mazungumzo yangu juu yake kwa yale ambayo yatafikia lengo lililokusudiwa, akipenda Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka. Basi Yeye peke yake ndiye anayeombwa msaada na uwezeshaji.

Suala la kwanza:

Sifa maalumu za Tauhidi na fadhila zake

Jua ya kwamba Tauhidi ina sifa maalumu na fadhila nyingi zinazoashiria hadhi yake ya juu na nafasi yake ya juu. Hapa, nitaashiria sifa kumi katika hizo:

Ya kwanza: Hakika ndiyo kusudi ambalo kwa ajili yake tuliumbwa na kuletwa ili tulitekeleze. Kama inavyoonyeshwa na maneno ya Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka: "Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi." [Suratu Dhariyat: 56]. Na maana ya: "ila waniabudu Mimi." Yaani wanipwekeshe. Kwa hivyo, Tauhidi ndiyo lengo tuliloumbwa kwa ajili yake katika maisha haya. Mwenyezi Mungu hakutuumba bure tu, wala hakutuacha bure na kututelekeza. Bali aliviumba viumbe ili vimuabudu na vimpwekeshe. Hilo linatosha kuwa ushahidi wa ukubwa wa jambo la Tauhidi na thamani yake ya hali ya juu.

Jambo la pili: Tauhidi ndiyo kiini cha wito wa Manabii na Mitume. Hili linamaanisha kwamba kila Nabii aliyetumwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu, basi wito wake uliegemezwa juu ya Tauhidi na kusimama juu yake. Kuna ushahidi mwingi juu ya hilo; ikiwa ni pamoja na kauli ya Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka: "Na kwa hakika, kwa kila umma tuliutumia Mtume ya kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na muepukeni Twaghuut (Shetani na vyote vinavyoabudiwa kinyume na Mwenyezi Mungu)." [An-Nahl: 36] Na amesema Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu mkubwa: "Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa tulimfunulia ya kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu." [Suratul-Anbiyaa: 25] Na amesema Mwenyezi Mungu, Mshindi, Mwenye nguvu: "Na waulize Mitume wetu tuliowatuma kabla yako: 'Je, tulifanya miungu mingine iabudiwe badala ya Rahmani (Mwingi wa rehema)?'" [Surat Az-Zukhruf: 45] Na akasema Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu mkubwa: "Na mtaje ndugu wa kina 'Adi, alipowaonya watu wake kwenye vilima vya mchanga. Na kwa yakini waonyaji wengi walitokea kabla yake na baada yake kuwaambia: Msimuabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu." [Al-Ahqaf: 21] Na annudhuru ni Mitume. Yaani, Mitume wa kabla na baada yake walikubaliana juu ya lengo hili. "Kwamba msiabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu." Kwa hivyo, kumpwekesha Mwenyezi Mungu ndicho kiini cha wito wa Manabii na Mitume. Kwa sababu ya hilo, neno la kwanza ambalo watu walisikia kutoka kwa Manabii wao, na jambo la kwanza walilowaanzisha kwalo katika suala la kulingania kwa Mwenyezi Mungu, ni kulingania kumpwekesha; kwa sababu ndio msingi ambao dini imejengwa juu yake. Kwani, mfano wa dini ni mfano wa mti. Na inavyojulikana ni kwamba mti una mizizi na matawi, nao hauwezi kunyooka katika mambo yake isipokuwa kwa mizizi yake. Dini pia haiwezi kunyooka isipokuwa kwa msingi wake. "Hivi hukuona vipi Mwenyezi Mungu alivyopiga mfano wa neno zuri? Ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara, na matawi yake yako mbinguni." [Surat Ibrahim: 24] Na kama vile mti unavyokufa ikiwa mizizi yake itakatwa, ndivyo pia dini ikiwa haitaegemezwa juu ya Tauhidi, basi haitawezekana kufaidika nayo.

Miongoni mwa yale yanayoashiria kuwa Tauhidi ndio kiini cha wito wa Manabii na Mitume na msingi wa ujumbe wao ni kauli ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, katika yale yaliyopokelewa kwa usahihi kutoka kwake: "Manabii ni ndugu wa baba mmoja, ila mama zao ni tofauti, na dini yao ni moja." [1] Yaani itikadi yao ni moja, kwa sababu wote walilingania kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Na "mama zao ni tofauti" inamaanisha sheria zao ndizo zilitofautiana. "Kila mmoja katika nyinyi tumemuwekea sheria yake na njia yake." [Al-Maida: 48]. Imepokelewa na Muslim, nambari (2365) kutoka katika Hadithi ya Abu Huraira, Mwenyezi Mungu amuwie radhi.

Jambo la tatu: Miongoni mwa sifa maalumu za Tauhidi ni kwamba hiyo ndiyo wajibu wa kwanza kwa mtu aliyewajibishwa na sheria. Kwa maana, jambo la kwanza ambalo mtu anatakiwa kulifanya ili kuingia katika dini hii ni Tauhidi, na jambo la kwanza ambalo mtu anaanza nalo katika kulingania kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Tauhidi. Hayo yanaashiriwa na ushahidi mwingi; ikiwa ni pamoja na: kauli ya Mtume- rehema na amani ziwe juu yake-: "Nimeamrishwa nipigane na watu mpaka waseme: Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu." Hadi mwisho wa hadithi ([2]) Na miongoni mwake ni yale ambayo Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, alimwambia Muadh ibn Jabal, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, alipomtuma Yemen: “Hakika wewe unawajia watu miongoni mwa watu wa Kitabu. Basi na liwe la kwanza utakalowalingania ni kumuabudu Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mtukufu." Hadi mwisho wa Hadithi [3]. Na katika riwaya nyingine, ilikuja kwa matamshi haya: “Hakika wewe unawajia watu miongoni mwa watu wa Kitabu. Basi na liwe la kwanza utakalowalingania ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu Mtukufu."[4] Na katika upokezi mwingine, ilikuja kwa matamshi haya: “Hakika wewe unawajia watu wa Kitabu. Basi utakapowajia, walinganie kushuhudia kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu."[5] Kwa hivyo, Tauhidi ndilo jambo la kwanza ambalo ni wajibu kwa wale wanaowajibika kisheria na wanaanzishwa kwalo. Nalo ndilo jambo la kwanza ambalo mtu anaingia kwalo katika dini hii. Hii ni kwa sababu Dini imesimama juu ya Tauhidi na ndiyo msingi ambao imejengwa juu yake. ( ) Imepokelewa na Bukhari (25, 1399) na Muslim (21, 22) kutoka katika Hadithi ya Abuu Huraira, bin Omari, na wengineo, Mwenyezi Mungu awe radhi nao. Imepokelewa na Bukhari (1458) na Muslim (19). (Imepokelewa na Bukhari (7372). (Imepokelewa na Bukhari (1496).

Jambo la nne: Miongoni mwa sifa maalumu za Tauhidi ni kwamba ndiyo amani na uongofu katika dunia na akhera. Soma hilo katika kauli ya Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka: "Wale walioamini, na hawakuchanganya imani yao na dhuluma, hao ndio wana amani, na wao ndio walioongoka." [Suratul An'am: 82]. Kwa hivyo, amani iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu, na Yeye, aliyetakasika na kutukuka, hampi amani hiyo ila mwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu kwa kumsafia dini. Aya hii ilipoteremka - kama ilivyoelezwa katika Hadithi Sahihi - jambo lake lilikuwa gumu kwa Maswahaba, Mwenyezi Mungu awawie radhi, wakamjia Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, na wakasema: Ni nani miongoni mwetu hajawahi kuidhulumu nafsi yake? Yaani: Hakuna hata mmoja wetu ambaye hajawahi kuidhulumu nafsi yake, na Mwenyezi Mungu anasema: "Wale walioamini, na hawakuchanganya imani yao na dhuluma, hao ndio wana amani, na wao ndio walioongoka?" Hilo linamaanasha kwamba hatuna fungu katika amani na uongofu. Kwa sababu kila mmoja wetu amewahi kuidhulumu nafsi yake. Basi Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, akasema: “Sivyo hivyo – yaani maana ya dhuluma katika Aya si hiyo-. Je, hamjasoma maneno ya mja mwema - Luqman Mwenye hekima? "Kwani hakika ushirikina bila ya shaka ni dhuluma kubwa." [Surat Luqman: 13] Hivyo basi – Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake – akaifasiri dhuluma katika Aya hii kuwa ni ushirikina. Basi muktadha huu unaonyesha kwamba yeyote anayeamini na asimshirikishe Mwenyezi Mungu; atakuwa na amani na uongofu duniani na akhera. Hizi ni miongoni mwa sifa maalumu za tauhidi; kwamba mwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu atampa amani na uongofu duniani na akhera.

Jambo la tano: Miongoni mwa sifa maalumu za Tauhidi ni kwamba haina mkanganyiko na mgongano, tofauti na imani nyinginezo, ambazo zina mikanganyiko na migongano. Hilo linaashiriwa na maneno ya Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka: "Kwani hawaizingatii hii Qur'ani? Na lau kuwa ingetoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, bila ya shaka wangelikuta ndani yake hitilafu nyingi." [Suratun Nisaa: 82] Hivyo basi, itikadi ambazo watu huzua na kuziunda zina mikanganyiko na migongano mingi. Ama imani sahihi, itikadi iliyo salama, Tauhidi madhubuti iliyothabiti inayotoka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, hiyo imesalimika kutokana na hayo yote.

Jambo la Sita: Miongoni mwa sifa maalumu za Tauhidi ni kwamba inakubaliana na maumbile yaliyo sawa na akili iliyonyooka. Tauhidi ndiyo dini ya maumbile, na kama mwanadamu angeachwa kwenye maumbile yake ya asili, asingekubali kitu kingine chochote isipokuwa Tauhidi. Kwa sababu inakubaliana na maumbile asili. Bali Tauhidi ndiyo maumbile ya asili, kama alivyosema Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka: "Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini kwa unyoofu, ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyonyooka sawa. Lakini watu wengi hawajui." [Surat Rum: 30]. Ama ushirikina, huo ni kutoka nje ya maumbile ya asili na kukengeuka mbali nayo. Ndiyo maana ilikuja katika Hadithi takatifu katika Sahihi Muslim, ambamo Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema: “Nami Hakika niliwaumba waja wangu wote huku wamenyooka sawasawa. Lakini waliwajia mashetani na wakawapoteza mbali na dini yao.” ([6]) Mimi niliwaumba waja wangu huku ni wanyoofu inamaanisha kwamba walikuwa kwenye maumbile ambayo ni Tauhidi. Kisha yakawajia mashetani na kuwapoteza mbali na dini yao. ( ) Imepokelewa na Muslim (2865) kutoka katika Hadithi ya 'Iyaadh ibn Himaar al-Mujashi’i, Mwenyezi Mungu amuwie radhi.

Na imepokelewa katika “Swahihi” kutoka katika Hadithi ya Abu Huraira, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, kwamba alisema: "Hakuna mtoto yeyote anayezaliwa isipokuwa anazaliwa katika maumbile ya asili. Kisha wazazi wake wanamfanya kuwa Myahudi au Mkristo au Mmajusi, kama mnavyozalisha wanyama. Je, huwa mnamkuta mnyama huyo akiwa amekatwa pua, mpaka muwe nyinyi ndio mnayemkata pua?" ([7]) Na katika riwaya, ilikuja hadithi hii hivi: "Kisha wazazi wake wanamfanya kuwa Myahudi au Mkristo au Mmajusi, kama anavyozalishwa mnyama akiwa mnyama mzima, je huwa mnahisi akiwa amekatika pua?" Mnyama hutoka katika tumbo la uzazi la mama yake akiwa mzima, akiwa na masikio, miguu na mikono kamili. Kisha anapokatika mguu, mkono, sikio au kitu kama hicho, basi hilo sio katika maumbile yake ya asili, lakini ni katika vitendo vya watu baada ya kuzaliwa akiwa kamili. Amesema Mtume, rehema na amani ziwe juu yake: "Mpaka muwe nyinyi ndio mnayemkata pua." Basi vivyo hivyo, mtoto mchanga anazaliwa kwenye maumbile ya asili, lakini anapobadilika akawa Mkristo, Myahudi, Mmajusi, au akaingia katika aina yoyote ya ukengeufu, upotofu na batili, basi hilo ni kwa sababu ya matendo ya wazazi wake au mazingira ambayo anakulia. (Imepokelewa na Bukhari (6599). (Imepokelewa na Bukhari (1358), na Muslim (2658).

Na kijana miongoni mwetu hukua *** katika yale waliyomzoesha wazazi wake.

Amesema Mtume, rehema na amani ziwe juu yake: "Kisha wazazi wake wanamfanya kuwa Myahudi, au Mkristo au Majusi (wanaoabudu moto)." Hakusema: “Au wanamsilimisha” kwa sababu alizaliwa katika maumbile ya asili na akakuwa katika hilo. Kwa hivyo Tauhidi ndiyo dini ya maumbile ya asili. Ama ushirikina na mambo mengineyo ya upotofu na batili, hayo yote yanapingana na maumbile ya asili na yako mbali sana nayo. Ama kuafikiana kwake na akili iliyonyooka, hilo ni kwa sababu akili iliyonyooka ambayo haijakengeuka au kupotoka hairidhii kitu kingine chochote isipokuwa Tauhidi. Basi ni nani huyu mwenye akili timamu na anaridhia kwamba kuna miungu wengi! Au kufungamana na makuba au udongo?! "Je, Miungu wengi tofautitofauti ni bora au Mwenyezi Mungu Mmoja Mwenye nguvu? 40. Hamuabudu badala yake isipokuwa majina tu mliyowaita nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuyateremshia hayo uthibitisho wowote. Hakuna hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu tu. Yeye ameamrisha msimuabudu yeyote isipokuwa Yeye tu. Hiyo ndiyo Dini iliyonyooka. Lakini wengi wa watu hawajui." [Surat Yusuf: 39-40]

Mmoja wa wale waliokuwa wakimpwekesha Mwenyezi Mungu katika zama za kabla ya Uislamu, Zaid bin Amr bin Nufail, alisema alipoiacha dini ya watu wake ([9]): () “As-Sirah” cha Ibn Ishaq (2/96).

Je, nitamuabudu mola mlezi mmoja au waola elfu moja*** mambo yanapogawanyika

Nimeshawaacha Al-Lat na Al-Uzza wote kwa pamoja*** hivyo ndivyo afanyavyo mstahamilivu mwenye subira mno

Basi sitamuabudu-Uzza wala binti zake wawili*** wala sitayazunguka yale masanamu mawili ya Banu Amr.

“Na alikuwa akiwashutumu Makuraishi kwa wanyama wao waliokuwa wakiwachinja (kwa ajili ya masanamu) na kusema: “Mwenyezi Mungu aliwaumba kondoo na akawateremshia maji kutoka mbinguni na akawaoteshea mimea kwenye ardhi, kisha mnawachinja kwa jina lisilokuwa la Mwenyezi Mungu." Aliyasema haya akiwapinga katika hilo na akiona kuwa ni jambo kubwa sana.([10]) () Sahihi Bukhari (3826).

Hakuna kitu katika akili kilicho bainifu zaidi au kilicho wazi zaidi kuliko kujua kwake ukamilifu wa Muumba wa ulimwengu huu, kutakasika kwake mbali na kasoro na mapungufu, na kwamba ni Yeye tu anayedhalilikiwa na kunyenyekewa. Na Mitume walikuja kwa ajili ya kukumbusha juu ya elimu hii na kuifafanua kwa undani. Kwa hivyo, uzuri wa Tauhidi na ubaya wa ushirikina viko imara katika akili na maumbile ya asili, na unajulikana kwa wale ambao wana nyoyo hai, akili timamu, na maumbile ya asili yaliyo sahihi.

Jambo la saba: Miongoni mwa sifa maalumu za Tauhidi ni kwamba Tauhidi ndiyo mafungamano ya kweli, yenye kudumu na yenye kuendelea katika dunia hii na akhera, na hakuna mafungamano baina ya watu hata kidogo kama mafungamano ya Tauhidi. Kwa sababu mafungamano haya baina ya watu wa Tauhidi na imani ni mafungamano ya kudumu, yenye kuendelea daima hapa duniani na akhera. "Siku hiyo, marafiki watakuwa ni maadui wao kwa wao, isipokuwa wachamungu." [Surat Az-Zukhruf: 67] Na amesema katika Aya nyingine: "... na yatakatika mafungamano yao." [Surat Al-Baqara: 166] Yaani, mahusiano na mafungamano yote yatakatika, kila upendo utatoweka, kila mawasiliano yataondoka isipokuwa upendo, mafungamano na mawasiliano ya kumpwekesha na kumuamini Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu Mtukufu. Kwa hivyo mafungamano yaliyokuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, hayo yatadumu na kuendelea kuungana. Na yale ambayo yalikuwa kwa ajili ya wengineo, yatakatika na kutenganishwa. Hivyo basi, haijalishi mafungamano ni ya nguvu kiasi gani, na mahusiano ni ya kina namna gani, yote hayo hakika yataisha katika dunia hii au akhera. Isipokuwa mafungamano ambayo yameegemezwa juu ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka, na kumuamini kwa uzuri. Mahusiano haya, ndiyo yatakayodumu na kuendelea kubakia hapa duniani na akhera.

Jambo la nane: Miongoni mwa sifa za Tauhidi ni usalama wa chanzo chake. Hii ni kwa sababu imechukuliwa kutoka kwenye chemchemi tamu na chanzo safi, kutoka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, Mwenye utukufu, na kutoka katika Sunna za Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ambaye hatamki kwa matamanio yake. Hayakuwa hayo ila ni ufunuo uliofunuliwa kwake. Tutakuja kuelezea upande huu kwa undani baadaye.

Jambo la tisa: Miongoni mwa sifa maalumu za Tauhidi ni uthabiti wake na kuhifadhiwa kwake. Kwa sababu Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka alichukua jukumu la kuihifadhi Tauhidi hii na dini hii na kuendelea kwake. "Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na Dini ya haki ili aipe ushindi juu ya dini zote, hata kama washirikina wakichukia." [Surat At-Tawba: 33], Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamini." [Al-Hajj: 38], Na akasema Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka: "Na ni wajibu juu yetu kuwanusuru waumini." [Surat Ar-Rum: 30]. Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Mwenyezi Mungu huwapa uthabiti wale walioamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na katika Akhera." [Ibrahim: 27].

Jambo la kumi: Miongoni mwa sifa maalumu za Tauhidi ni kwamba inajumuisha matunda mengi, fadhila nyingi na athari mbalimbali katika dunia na akhera. Tutazungumza juu ya baadhi ya hayo mwishoni mwa mada hii.

Suala la pili:

Maana ya Tauhidi na uhakika wake

Neno 'Tauhidi' ni jina linalotokana na kitenzi 'wahhada, yuwahhidu, tawhiidan', ambacho ni mzizi unaoashiria upweke na umoja. Na kumpwekesha Mwenyezi Mungu ni kumfanya Yeye aliyetakasika na kutukuka kuwa peke yake na kumkanushia mshirika yeyote katika haki zake na sifa zake maalumu. Kwa hivyo, hana mshirika yeyote katika mambo yake mahususi, wala katika haki zake zozote zilizoko juu ya waja wake.

Nao umola ni kuendesha ulimwengu huu katika suala la uumbaji, utoaji riziki, kuhuisha, kufisha na kusimamia mambo. Hayo yote ni katika mambo mahususi ya Mwenyezi Mungu.

Pia ni katika mambo yake mahususi: Majina yake mazuri, sifa zake za juu zaidi, utashi wake wenye kutekelezeka, uwezo wake unaojumuisha kila kitu, elimu yake pana na ukamilifu wake Yeye mwenye utukufu mkubwa katika majina na sifa zake. Kwa hivyo, atakayenasibisha kiumbe chochote na chochote katika mambo mahususi ya Mwenyezi Mungu, atakuwa ameivunja Tauhidi yake kwa hilo.

Haki za Mwenyezi Mungu juu ya waja wake ni kwamba wamuabudu na wasimshirikishe na chochote, kama ilivyo katika hadithi ya Muadhi, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, Mtume, rehema na amani zimshukie, alisema kumwambia: "Ewe Muadhi! Je, unajua ni ipi haki ya Mwenyezi Mungu juu ya waja wake? Na ni ipi haki ya waja juu ya Mwenyezi Mungu?" Akasema: Nikasema: 'Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndio wanaojua zaidi.' Akasema: "Basi hakika haki ya Mwenyezi Mungu juu ya waja wake ni kumuabudu Mwenyezi Mungu na kutomshirikisha na chochote. Na haki ya waja juu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kwamba asimuadhibu ambaye hamshirikishi na chochote." Hivyo basi, ibada ni haki ya Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka. Yeyote atakayemfanyia asiyekuwa Mwenyezi Mungu ibada yoyote ile, basi ameivunja Tauhidi yake kwa hilo. Imepokelewa na Bukhari (2856, 5967) na Muslim (30).

Basi Tauhidi ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu Mtukufu katika haki zake na mambo yake mahususi. Na ushirikina ni kumsawazisha asiyekuwa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu katika chochote miongoni mwa haki zake au mambo yake mahususi. Huu ndio uhakika wa Tauhidi: kwamba tumpwekeshe Mwenyezi Mungu Mtukufu aliyetakasika na kutukuka, na kwamba tusimfanyie mshirika, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mtukufu: "Na muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote." [An-Nisaa: 36] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na Mola wako Mlezi amehukumu kuwa msimuabudu isipokuwa Yeye tu." [Al-Israa: 23] Na akasema Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka: "Na hawakuamrishwa ila wamuabudu Mwenyezi Mungu, wakimtakasia Dini yao." [Al-Bayyina: 5] Na kuna aya nyingi zenye maana hii.

Hivyo basi, inadhihirika kwa hilo kwamba Tauhidi ina sehemu tatu: Tauhidi ya Umola, Tauhidi ya majina na sifa na Tauhidi ya Uungu.

Ama Tauhidi ya Umola, hiyo ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka, kwa kuamini kwamba Yeye pekee ndiye Muumba, Mtoaji riziki, Mmiliki, Mneemeshaji, Mwendeshaji mambo, ambaye hana mshirika katika lolote miongoni mwa hayo. "Sema: 'Ni nani Mola Mlezi wa mbingu na ardhi?' Sema: Mwenyezi Mungu." [Ar-Ra`d: 16]. Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Sema: 'Ni ya nani ardhi na viliomo ndani yake, kama nyinyi mnajua?' Watasema: 'Ni vya Mwenyezi Mungu!' Sema: 'Basi, je, hamkumbuki?' Sema: 'Ni nani Mola Mlezi wa mbingu saba na Mola Mlezi wa 'Arshi Kuu?' Watasema: 'Ni vya Mwenyezi Mungu.' Sema: 'Basi je, hamchi?' Sema: 'Ni nani mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu, naye ndiye anayelinda, wala hakilindwi asichotaka, kama mnajua?' Watasema: '(Ufalme huo) ni wa Mwenyezi Mungu.' Sema: 'Basi vipi mnadanganyika?" [Surat Al-Mu'minun: 84-88] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Huyo ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote." [Surat Ghafir: 64] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu, na Yeye ni Mmiliki wa kila kitu." [Surat Az-Zumar: 64] Na aya zinginezo.

Sehemu ya pili: Kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika majina na sifa zake. Huku ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu Mtukufu aliyetakasika na kutukuka katika majina yake mazuri mno na sifa zake tukufu zilizotajwa katika Kitabu chake na Sunna za Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye tu. Yeye ana majina mazuri kabisa." [Surat Twaha: 8] Na akasema Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka: "Sema: Muombeni Mwenyezi Mungu au muombeni Mwingi wa Rehema, kwa [jina] lolote mnalomuita. Kwani Yeye ana majina mazuri mazuri kabisa." [Al-Isra: 110] Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, ambaye hapana mungu isipokuwa Yeye tu. Mwenye kuyajua yaliyofichikana na yanayoonekana. Yeye ndiye Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. Yeye ndiye Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipokuwa Yeye tu. Mfalme, Mtakatifu, Mwenye salama, Mtoaji wa amani, Mwenye kuyaendesha Mwenyewe mambo yake, Mwenye nguvu, Anayefanya analolitaka, Mkubwa. Ametakasika Mwenyezi Mungu mbali na hayo wanayomshirikisha nayo. Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Muumbaji, Mtengenezaji, Mtia sura, Mwenye majina mazuri kabisa. Kila kilichoko katika mbingu na ardhi kinamtakasa, naye ni Mwenye kushinda, Mwenye hekima." [Surat Al-Hashr: 22-24].

Sehemu ya tatu: Tauhidi ya uungu. Ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka katika ibada, kama vile dua, matumaini, hofu, nadhiri, kuchinja, swala, funga na ibada nyinginezo, na kumsafia dini Yeye peke yake na kujitenga na ushirikina, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na hawakuamrishwa ila wamuabudu Mwenyezi Mungu, wakimtakasia Dini yao." [Al-Bayyina: 5] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hakika Dini iliyo safi ni ya Mwenyezi Mungu." [Az-Zumar: 3]. Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Sema: Hakika Swala yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote. Hana mshirika, na hili nimeamrishwa." [Surat Al-An'am: 162-163] Amesema Mtume, rehema na amani zimshukie: "Mwenye kufa na huku anaomba mwenza kinyume na Mwenyezi Mungu, ataingia Motoni." ([12]) Hii ndiyo Tauhidi na huu ndio uhakika wake. ( ) Imepokelewa na Bukhari (4497) na matamshi haya ni yake, na Muslim (92) kwa kutoka katika hadithi ya Abdullah bin Masud, Mungu amuwie radhi.

Kila moja kati ya sehemu hizi tatu ina kinyume chake. Kwa hivyo, unapokwishajua kwamba Tauhidi ya Umola ni kukiri kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Muumba, Mtoa riziki, Mhuishaji, Mfishaji, Msimamizi wa mambo yote, Mwendeshaji wa viumbe vyake vyote, na kwamba hana mshirika katika ufalme wake; basi kinyume cha hili ni mja kuitakidi kuwepo kwa yule anayeweza kuendesha mambo pamoja na Mwenyezi Mungu katika mambo ambayo hayawezi isipokuwa Mwenyezi Mungu tu.

Na unapokwishajua kuwa Tauhudi ya majina na sifa ni Mwenyezi Mungu kuitwa kwa jinsi alivyojiita mwenyewe, na kuelezewa kwa yale aliyojielezea mwenyewe, na namna alivyomuelezea Mtume wake Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake,  na akanushiwe kufananishwa na kupigiwa mifano, basi kinyume cha hayo ni mambo mawili, ambayo yanajumuishwa katika neno ukataajimungu:

La kwanza: Kumkanushia Mwenyezi Mungu Mtukufu hayo, na kukataa sifa za ukamilifu wake, na maelezo ya utukufu wake ambayo yalithibiti katika Kitabu na Sunna.

La pili: Kufananisha sifa za Mwenyezi Mungu na sifa za viumbe vyake. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona." [Surat Ash-Shura: 11] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Yeye anajua yaliyo mbele yao, na yaliyo nyuma yao. Wala wao hawawezi kumjua Yeye vilivyo." [Twaha: 110].

Na unapokwishajua kwamba Tauhidi ya Uungu ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kila aina ya ibada, na kukikanushia ibada kitu kisichokuwa Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka, basi kinyume cha hayo ni kumfanyia ibada yoyote asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mtukufu, na hili ndilo lililoenea miongoni mwa washirikina wengi, na ndilo lililokuwa na mzozo kati ya Mitume wote na umma zao. ([13]) () “Ma'arij Al-Qabuul" cha Sheikh, Al-Hafidh Al-Hakamii (1/418).

Suala la tatu:

Kutekeleza na kukamilisha Tauhidi

Kutekeleza tauhidi ni daraja ya juu, na ni cheo cha juu, na ni kiwango kitukufu. Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, alisema kuwa watu wake wataingia Peponi Siku ya Kiyama bila ya hesabu wala kuadhibiwa katika hadithi mashuhuri ya bin Abbas na wengineo, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, kwamba alisema: "Na pamoja nao wapo sabini elfu watakaoingia Peponi bila ya hesabu wala adhabu." Kisha akawataja katika kauli yake: "Hao ndio wasiofanya ruqya, wala hawatafuti kufanyiwa ruqya, wala hawaathiriki na vitu kama vile ndege (bundi), na wanamtegemea Mola wao Mlezi." Basi hii ndiyo daraja ya juu ya Tauhidi, ambayo ni kutekeleza Tauhidi sawasawa na kuikamilisha. Imepokelewa na Bukhari (5705) na Muslim (220).

Kutekeleza Tauhidi kunamaanisha kukamilisha tauhidi sawasawa, kuisafisha na kuitakasa kutokana na uchafu wa ushirikina, uzushi na maasi. Mambo haya matatu yanaitwa na wanazuoni: vizuizi vinavyomzuia mwenye kutembea katika njia yake ya kwenda kwa Mwenyezi Mungu na nyumba ya Akhera: kizuizi cha ushirikina, kizuizi cha uzushi na kizuizi cha maasi.

Ama kizuizi cha ushirikina; Wokovu kutokana nao ni kwa kumpwekesha Mwenyezi Mungu sawasawa. Na ama kizuizi cha uzushi; hicho mtu anaokoka kutokana nacho kwa kushikamana na Sunna, kumfuata Mtume, Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, na kutembelea katika njia yake. Na ama ili kuokoka kutokana na kizuizi cha maasi, mtu anapaswa kujiweka mbali nayo, kutahadhari kutumbukia humo, kutubia toba ya kweli kwa Mwenyezi Mungu ikiwa ataanguka katika dhambi na uasi wowote. Kwa hivyo, ikiwa mja yuko katika kiwango hiki, basi ameshatekeleza Tauhidi sawasawa.

Na kutekeleza Tauhidi sawasawa pia kuna viwango viwili: Utekelezaji wa faradhi na utekelezaji unaopendekezwa. Watu wote wa viwango hivi viwili wataingia Peponi Siku ya Kiyama bila ya hesabu wala adhabu.

Kiwango cha kwanza cha kutekeleza Tauhidi ni kiwango cha watu wa katikati. Nao ni wale wanaofanya mambo ya wajibu na kujiepusha na yale yaliyoharamishwa. Kwa hivyo, ikiwa mja yuko katika hali hii, akitunza wajibu na faradhi na kujiepusha na maharamisho, madhambi makubwa na maasi, basi atakuwa ametekeleza Tauhidi sawasawa kwa njia ya wajibu, na anakuwa miongoni mwa walio katikati, na wao ni miongoni mwa wale watakaoingia Peponi bila ya hesabu wala adhabu. Hiki ni kiwango kimoja.

Kiwango cha pili kiko juu zaidi kuliko kiwango hiki, ambacho ni kutekeleza Tauhidi inayopendekezwa. Na hiki ndicho kiwango cha waliotangulia katika mambo ya kheri. Hao ni wale ambao licha ya kuhifadhi na kutunza kwao mambo ya faradhi na kujiepusha na madhambi makubwa na vitendo vilivyoharamishwa, wanashindana katika vitendo vinavyotamanika, vya kujitolea na vinavyopendekezwa.

Watu hawa ambao waliotekeleza Tauhidi sawasawa katika makundi yao yote mawili - walio wastani na wale waliotangulia katika mambo ya kheri - wote wataingia Peponi Siku ya Kiyama bila ya kuhesabiwa wala kuadhibiwa. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema: "Kisha tumewarithisha Kitabu hao ambao tuliwateua miongoni mwa waja wetu. Kati yao yupo aliyejidhulumu, na yupo wa katikati, na yupo aliyetangulia katika mambo ya heri, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo fadhila kuu. Mabustani ya milele watayaingia." [Surat Fatir: 32-33] Yaani makundi haya matatu yataingia katika Bustani za milele: waliojidhulumu nafsi zao, wa katikati na wanaotangulia katika mambo ya kheri.

Ama wa katikati na wanaotangulia katika mambo ya kheri, hao kuingia kwao Peponi ni kuingia moja kwa moja bila ya hesabu.

Na ama waliojidhulumu nafsi zao kwa madhambi yaliyo chini ya ushirikina, basi wataingia Peponi, lakini hawataingia humo moja kwa moja bila ya hesabu wala adhabu, sawa na wale watu wa kati na kati na wanaotangulia katika mambo ya kheri. Bali wanaweza kuadhibiwa na kufanyiwa hesabu, nao watakuwa chini ya mapenzi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, akitaka atawaadhibu, na akitaka atawasamehe.

Suala la Nne:

Mambo yanayobatilisha Tauhidi na kuipunguza

Tauhidi ina mambo yanayoibatilisha na kuipunguza. Mambo yanayoibatilisha Tauhidi ni yale yanayoharibu matendo na kubatilisha dini nzima. Nayo ni kumkufuru Mwenyezi Mungu, ushirikina na unafiki halisi. Ukafiri kwa aina zake zote na ushirikina kwa aina zake zote, na unafiki mkubwa kwa aina zake zote, vyote hivyo vinabatilisha Tauhidi kutokea kwenye asili yake na kuibomoa kwenye msingi wake. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka ya chini kabisa Motoni." [An-Nisaa: 145], Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na anayekataa kuamini, bila shaka matendo yake yameharibika." [Al-Ma’idah: 5], Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na kwa yakini yamefunuliwa kwako na kwa wale waliokuwa kabla yako: Bila ya shaka, ukimshirikisha Mwenyezi Mungu yataporomoka matendo yako, na lazima utakuwa miongoni mwa wenye kupata hasara." [Surat Az-Zumar: 65] Kwa hivyo, Tauhidi inaharibika, inabomoka na kubatilika kwa aina zote za ushirikina mkubwa, aina zote za unafiki mkubwa na aina zote za ukafiri mkubwa. Hayo yote yanachukua muda mrefu kuyazungumzia na kutaja maelezo yake kwa kina.

Ama vinavyopunguza Tauhidi, ni mambo yanayopunguza lakini hayaibatilishi au kuibomoa kutokea kwenye msingi wake. Miongoni mwake ni ukafiri mdogo na unafiki wa kivitendo, kama vile yale yaliyotajwa katika Hadithi hii: “Alama za mnafiki ni tatu: Anapozungumza husema uongo. Na anapotoa ahadi, huivunja. Na anapoaminiwa, hufanya hiyana.” ([15] Mambo haya yanayopunguza Tauhidi yanapopatikana kwa mja, inapungua Tauhidi yake na imani yake. Vile vile ushirikina mdogo na matamshi ya kishirikina ambayo mtu hakukusudia uhakika wake, bali yanatokea tu katika ulimi wake. Haya yanapunguza tu Tauhidi yake. Ama ikiwa ataitakidi uhakika wake, basi yatakuwa katika ushirikina mkubwa unaobatilisha Tauhidi. () Imepokelewa na Bukhari (33), na Muslim (58) kutoka katika Hadithi ya Abuu Huraira.

Kwa hivyo, Muumini hana budi kuchunga Tauhidi yake na kuwa makini nayo kwa kuiweka mbali na kila kinachoibatilisha na kuipunguza.

Sheikh, Abdul Rahman bin Hassan alisema: “Jua ya kwamba kinyume cha Tauhidi ni ushirikina. Nao ni aina tatu: Ushirikina mkubwa, ushirikina mdogo na ushirikina uliofichika.

Ushahidi wa ushirikina mkubwa ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kushirikishwa na kitu. Lakini Yeye husamehe yasiyokuwa hayo kwa amtakaye. Na anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, basi huyo amepotea upotovu wa mbali." [Surat An-Nisaa: 116], Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na Masihi mwenyewe alisema: 'Enyi Wana wa Israeli! Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi. Kwani anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu atamharamishia Pepo, na mahala pake ni Motoni. Na waliodhulumu hawatakuwa na wale wa kuwanusuru." [Surat Al-Ma'idah: 72].

Na ushirikina ni aina nne:

Aina ya kwanza: Ushirikina katika kuomba. Na ushahidi wake ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na wanapopanda katika Safina na Majahazi, humuomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafia utiifu. Lakini anapowavusha wakafika nchi kavu, mara wanamshirikisha. Wapate kuyakana tuliyowapa, na wajistareheshe. Lakini watakuja jua!" [Surat Al-Ankabut: 65-66].

Aina ya pili: Ushirikina katika nia. Nao huwa katika utashi na makusudio, na ushahidi wake ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Wale wanaotaka maisha ya dunia na pumbao lake, tutawalipa humo vitendo vyao kamili. Na wao humo hawatopunjwa. Hao ndio ambao hawatakuwa na kitu Akhera ila Moto, na yataharibika waliyoyafanya, na yatapotea bure waliyokuwa wakiyatenda." [Surat Hud: 15-16].

Aina ya tatu: Ushirikina katika utiifu, na ushahidi wake ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Waliwafanya makuhani wao na Makasisi wao kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu, na pia Masihi bin Maryamu. Na wala hawakuamrishwa isipokuwa wamuabudu Mungu Mmoja, hapana mungu ila Yeye. Sub-hanahu (ametakasika) mbali na hayo wanayomshirikisha nayo." [Surat At-Tawba: 31] Tafsiri yake ambayo haina tatizo ni kwamba hilo huwa kwa kuwatii wanachuoni na wale wafanyao ibada mno miongoni mwao katika yale ambayo wanamuasi Mwenyezi Mungu Mtukufu, na sio kuwaomba wao dua, kama Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, alivyomfasiria aya hii 'Adi bin Hatim, alipomuuliza, akisema: "Sisi hatuwaabudu." Basi akamtajia kuwa kuwaabudu ni kuwatii katika yale wanayomuasi Mwenyezi Mungu.

Aina ya nne: Ushirikina katika mapenzi, na ushahidi wake ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na katika watu wapo wanaochukua waungu wasiokuwa Mwenyezi Mungu. Wanawapenda kama kumpenda Mwenyezi Mungu. Lakini walioamini wanampenda Mwenyezi Mungu zaidi sana. Na laiti waliodhulumu wakajuwa watakapoiona adhabu kuwa nguvu zote ni za Mwenyezi Mungu na kuwa Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu!" Hadi kauli yake: "Wala hawatakuwa wenye kutoka Motoni." [Surat Al-Baqara: 65-67].

Aina ya pili: Ushirikina mdogo, ambao ni kujionyesha, na ushahidi wake ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Kwa hivyo, mwenye kutaraji kukutana na Mola wake Mlezi, basi na atende vitendo vyema, wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya Mola wake Mlezi." [Surat Al-Kahf: 110].

Aina ya tatu: Ushirikina uliofichika, na ushahidi wake ni kauli ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake: "Ushirikina katika umma huu umefichika zaidi kuliko kutambaa kwa mdudu chungu kwenye jiwe jeusi katika giza la usiku." Na kafara yake aliisema Mtume, rehema na amani ziwe juu yake: “Ewe Mwenyezi Mungu, hakika mimi najikinga kwako nisikushirikishe na chochote na hali ninajua, na ninakuomba msamaha kwa dhambi nisiyoijua.”

Nao ukafiri una aina mbili:

Ukafiri ambao unamtoa mtu katika mila ya Uislamu, nao ni aina tano:

Aina ya kwanza: Ukafiri wa kukanusha, na ushahidi wake ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayemzulia uongo Mwenyezi Mungu au anayekanusha Haki inapomjia? Je, si katika Jahannamu ndio yatakuwa makazi ya makafiri?" [Surat Al-Ankabut: 68].

Aina ya pili: Ukafiri wa kufanya kiburi na kukataa lakini pamoja na kusadikisha, na ushahidi wake ni kauli yake: "Na tulipowaambia Malaika: 'Msujudieni Adam', wakamsujudia wote isipokuwa Iblisi, alikataa na akajivuna na akawa katika makafiri." [Surat Al-Baqara: 34].

Aina ya tatu: Ukafiri wa shaka, ambao ni ukafiri wa dhana, na ushahidi wake ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na akaingia kwenye Bustani yake, naye hali anajidhulumu nafsi yake. Akasema: 'Sidhani kabisa kuwa haya yataharibika. Wala sidhani kuwa hiyo Saa (ya Kiyama) itatokea. Na ikiwa nitarudishwa kwa Mola wangu Mlezi, bila ya shaka nitapata marejeo bora zaidi kuliko haya. Mwenzake akamwambia kwa kubishana naye: 'Je, unamkufuru aliyekuumba kutokana na udongo, tena kutokana na tone la manii, kisha akakufanya mtu kamili?'" [Surat Al-Kahf: 35-37].

Aina ya nne: Kufuru ya kupuuza, na ushahidi wake ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na wale waliokufuru wanayapuuza yale wanayoonywa." [Surat Al-Ahqaf: 3].

Aina ya tano: Ukafiri wa unafiki, na ushahidi wake ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hayo ni kwa sababu ya kuwa waliamini, kisha wakakufuru; kwa hivyo zimezibwa nyoyo zao. Kwa hivyo hawafahamu lolote." [Surat Al-Munafiqun: 3].

Na ukafiri mdogo ambao haumtoi mtu nje ya Uislamu, nao ni kukufuru neema. Ushahidi wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mji uliokuwa na amani na utulivu, riziki yake ikiufikia kwa nafasi kutoka kila mahali. Lakini ukazikufuru neema za Mwenyezi Mungu; kwa hivyo Mwenyezi Mungu akauvisha vazi la njaa na hofu kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyafanya." [An-Nahl: 112], Na kauli yake: "Hakika mwanadamu ni dhalimu mkubwa, mwenye kuzikufuru mno neema." [Surat Ibrahim: 34].

Na ama unafiki, huo una aina mbili: Unafiki wa kiitikadi na unafiki wa kimatendo.

Ama unafiki wa kiitikadi:

Huo una aina sita:

Kama vile kumkanusha Mtume, au kukanusha baadhi ya yale aliyoyaleta Mtume, au kumchukia Mtume, au kuchukia aliyoyaleta Mtume, au kufurahishwa na kuporomoka kwa dini ya Mtume, au kuchukia ushindi wa dini ya Mtume. Aina hizi sita, mwenye kusifika kwazo ni miongoni mwa watakaokuwa katika tabaka la chini kabisa katika Moto, na tunajikinga kwa Mwenyezi Mungu tusije tukawa waovu na wanafiki.

Ama unafiki wa kivitendo:

Huo una aina tano:

Akizungumza, anasema uongo. Na akizozana, anapindukia mipaka. Na anapoagana agano, analifanyia usaliti. Na anapoaminiwa, hufanya hiyana. Na anapoahadi, anaivunja ahadi. Na Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye zaidi." ([16]). () “Ad-Durar Assaniyya” (3/66).

Suala la Tano:

Chanzo cha Tauhidi na chimbuko lake

Tauhidi ni Dini sahihi na imani thabiti inayotokana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume wake, rehema na amani ziwe juu yake, na ndiyo dini pekee iliyoteremshwa na ufunuo kutoka mbinguni. Itikadi zote walizo nazo watu zinazopingana na Tauhidi na kwenda kinyume nayo, hizo ni itikadi zilizoota kutoka katika ardhi ambazo watu walizizua na kuzitengeneza. Kwa hivyo, Tauhidi ndiyo itikadi ya pekee iliyoshuka kutoka mbinguni kupitia wahyi wa Mwenyezi Mungu, na ndiyo dini ya Mwenyezi Mungu aliyoichagua kwa ajili ya waja wake. "....na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini." [Al-Ma’idah: 3], Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na anayetafuta dini isiyokuwa Uislamu, haitakubaliwa kutoka kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kupata hasara." [Surat Al Imran: 85], Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na nani atajitenga na mila ya Ibrahim isipokuwa anayeitia nafsi yake katika upumbavu?" [Al-Baqarah: 130], Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hakika Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu." [Al Imran: 19]; Kwa hivyo, Tauhidi ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu aliouteremsha kwa waja wake. Nayo ndiyo Dini ya Mwenyezi Mungu ambayo kwa ajili yake aliwaumba viumbe na kuwafanya kuwepo ili waitekeleze, ndiyo maana tulishasoma kauli hii ya Mwenyezi Mungu hapo awali: "Na tulikwisha tuma kwa kila umma Mtume kuwaambia: Muabuduni Mwenyezi Mungu na jiepusheni na Twaghut (miungu ya uongo)." [An-Nahl: 36], "Amri ya Mwenyezi Mungu itakuja tu, basi msiiharakishe. Ametakasika na kutukuka mbali na hayo wanayomshirikisha nayo. Huwateremsha Malaika na Roho kwa amri yake juu ya amtakaye katika waja wake ili nyinyi muonye kwamba hapana mungu ila Mimi, basi nicheni Mimi." [Surat An-Nahl: 1-2].

Ama itikadi zisizokuwa Tauhidi, hizo ni itikadi zilizoota kutoka kwenye ardhi, zilizozuliwa na kutengenezwa na watu. Ndiyo maana ilikuwa katika mbinu za Mitume katika kubatilisha itikadi walizo nazo watu miongoni mwa ushirikina, ukafiri, unafiki na aina nyinginezo za upotofu ilikuwa ni kueleza kwamba hakuna wahyi ulioshuka juu ya itikadi hizo. Na tulishasoma kauli ya Nabii Yusuf akiwaambia wale wenzake wawili waliokuwa pamoja naye katika gereza: "Je, mabwana wengi wanaofarikiana wao kwa wao ni bora au Mwenyezi Mungu Mmoja Mwenye nguvu? Hamuabudu badala yake ila majina tu mliyowapa nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuyateremshia hayo uthibitisho wowote." [Surat Yusuf: 39-40], Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema katika Surat An-Najm: "Je, mmemuona Lata na Uzza? Na Manaat, mwingine wa tatu? Je, nyinyi mnao wana wanaume na Yeye ndio awe na wanawake? Huo basi ni mgawanyo wa kidhuluma! Hayo hayakuwa ila ni majina mliyowapa nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuleta uthibitisho wowote juu ya hayo." [Surat An-Najm: 19-22] Na Huud, amani iwe juu yake, aliwaambia watu wake: "Mnabishana nami kwa ajili ya majina tu mliyoyaita nyinyi na baba zenu ambayo kwayo Mwenyezi Mungu hakuteremsha uthibitisho? Basi ngojeni, mimi hakika pia ni pamoja nanyi katika wanaongoja." [Surat Hud: 71].

Kwa hivyo, Tauhidi chanzo chake na chimbuko lake ni kutoka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu na Sunna za Mtume wake, rehema na amani ziwe juu yake. Ilichukuliwa kutoka katika rasilimali hii tamu na chemchemi safi. Ama itikadi walizo nazo watu, chanzo chake ima ni yale ambayo akili zao potovu zinawaamuru na kuelekezwa kwazo na rai zao mbovu, au ni ufunuo kutoka kwa mashetani wao waasi. Na Ufunuo una aina mbili: Ufunuo kutoka kwa Mwingi wa Rehema na ufunuo kutoka kwa Shetani. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na kwa yakini mashetani wanawafunulia ufunuo marafiki zao kubishana nanyi. Na mkiwafuata, basi hapana shaka nyinyi mtakuwa washirikina." [Surat Al-An'am: 121] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na kadhaalika tumemfanyia kila Nabii maadui mashetani wa kibinadamu, na kijini, wakifundishana wao kwa wao maneno ya kupambapamba ya udanganyifu." [Al-An’am: 112], Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Je, nikwambieni ni nani wanaoshukiwa na Mashetani?" [Surat Ash-Shu'ara': 221] Al-Mukhtar bin Abi Ubaid alikuwa wa aina hii, kiasi kwamba ilisemwa kwa bin Omari na bin Abbas, mmoja wao akaambiwa: 'Hakika, anasema kuwa anafunuliwa ufunuo.' Akasema: "Na kwa yakini mashetani wanawafunza marafiki zao kubishana nanyi." Na akaambiwa huyo mwingine: 'Hakika, anasema kuwa anafunuliwa ufunuo.' Akasema: "Je, nikwambieni nani wanaoshukiwa na Mashetani?" () “Majmu'ul Fataawa” cha bin Taimiya (13/75).

Kwa hivyo, Shetani huwafunulia ufunuo watu wapotofu kwa itikadi, mawazo, wasiwasi na fikira wanazoziamini, kisha huwalingania watu katika hayo kwa ufunuo huo uliowashukia kutoka kwa Shetani, au mambo ambayo mtu huyafikia kwa ladha yake ya upotovu. Kisha kutokana na hayo hutokea matendo, ibada na matambiko mbalimbali, na wanasema katika kuwatolea ushahidi: "Haya ni kutokana na tajiriba yetu au tajiriba ya mashekhe wetu." Lakini Dini haichukuliwi kutokana na tajiriba au matendo wanayoyachukua kutoka katika ndoto. Pia wao husema: "Niliona hivi na hivi katika ndoto." kisha anajenga dini au itikadi juu yake, na kadhalika kutoka kwenye vyanzo ambavyo watu wengi wanatoa hapo itikadi ambazo Mwenyezi Mungu, Mwenye baraka nyinyi, Mtukufu hakuziteremshia uthibitisho wowote.

Hivyo basi, itikadi iliyobarikiwa ni itikadi ya Tauhidi, ambayo ndiyo dini ya Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu haikubali dini yoyote isipokuwa hiyo. Hii ni itikadi inayotokana na chanzo kitamu na chemchemi safi, na atakayechukua kutoka kwenye chanzo cha kwanza na chemchemi tamu, atapata chemchem nyinginezo zikiwa mbovu na zilizochafuliwa. Lakini, mtu hawezi kujua kuchafuliwa kwa vyanzo hivi isipokuwa atakapojua chemchemi iliyo safi kabisa ambayo ni ufunuo wa Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka na uteremsho wake. Basi ndiyo maana utawaona washirikina wengi baada ya kuongoka na kuingia kwao katika Tauhidi, wanabainikiwa kuwa walikuwa watu wasiotumia akili, ilhali wakati walipokuwa katika upotofu wao, ushirikina wao na batili yao, walidhani kuwa hali waliyomo ndiyo hali ya kuwa na akili sahihi na dini iliyonyooka.

Ndiyo maana baadhi ya Maswahaba walikuwa wanakaa na kutaja baadhi ya hadithi zao za ajabu walipokuwa washirikina na wanamtukuza Mwenyezi Mungu aliyewaongoza kuingia katika Uislamu na Tauhidi. Imesimuliwa kutoka kwa Abu Othman an-Nahdi – ambaye aliishi zama za kabla ya Uislamu na akasilimu katika zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, lakini hakumuona – alisema: “Tulikuwa tukiabudu jiwe katika zama za kabla ya Uislamu, na tukamsikia muitaji akiita: 'Enyi watu walio safarini! Hakika mola wenu mlezi ameshaangamia, basi mtafuteni mola mlezi mwingine - akimaanisha kwamba lile jiwe walilokuwa nalo walilokuwa wakiliabudu lilipotea.' Akasema: 'Basi tukatoka tukaenda kwenye kila njia ngumu na nyepesi, na mara tulipokuwa tunalitafuta, tukamsikia muitaji akiita: 'Hakika tumempata mola wenu mlezi' au mfano wake. Akasema: 'Basi tukaja, na tazama, kulikuwepo na jiwe jingine. Kwa hivyo, tukalichinjia ngamia wetu juu yake.' Yaani, walipata jiwe jingine mfano wa jiwe lile la kwanza au jiwe linalokaribiana na hilo. Kwa hivyo, wakaja nalo, wakalielekea wakiliabudu, wakilitaraji na kulielekezea dua, matumanini na vichinjo. Basi ziko wapi akili za watu hawa?! Imepokelewa na bin Abi Shaiba katika “Musannaf” (33914), Ibn Sa’d katika “At-Twabaqaat Al-Kubra” (7/97), na Abu Nu'aim katika “Ma’rifat As-Sahaba” (4707), na mlolongo wa upokezaji wake ni mzuri.

Hata hivyo, wakati walipokuwa wanafanya vitendo hivi na mambo haya, walikuwa wakiwaelezea Manabii na Mitume wa Mwenyezi Mungu kwamba wao ni wendawazimu na wanajiona wenyewe kwamba ndio wenye akili timamu. Lakini wakati Mwenyezi Mungu mwenye utukufu mkubwa anapoangaza ufahamu kwa Tauhidi na imani na Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mtukufu akaziongoa nyoyo kuingia katika Uislamu, inamdhihirikia mtu ubovu wa kile ambacho washirikina wapo juu yake na kwamba hivyo vyanzo ambavyo walivitegemea vilichafuliwa na kuchanganyika na kila batili na upotovu, na inadhihirika wazi kwamba kila mshirikina ni mbovu wa akili.

Suala la Sita:

Matunda na faida za Tauhidi

Tauhidi ina matunda yasiyohesabika na faida ambazo haziwezi kudhibitiwa. Tazama namna kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu alivyoashiria hayo: "Hivi hukuona vipi Mwenyezi Mungu alivyopiga mfano wa neno zuri? Ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara, na matawi yake yako mbinguni. Hutoa matunda yake kila wakati." [Surat Ibrahim: 24-25] Yaani hutoa matunda na faida zake.

Kwa hivyo, faida za Tauhidi na matunda yake kwa mja katika dunia yake na akhera yake hayana kikomo na hayazuiliki. Bali tutasema tu kauli ya ujumla:

Hakika, kila kheri anayoipata mja duniani na akhera, na kila shari ambayo mja anaepushwa mbali nayo duniani na akhera, ni kutokana na matunda ya Tauhidi na athari katika athari zake. Kwani, miongoni mwa matunda makubwa zaidi ya Tauhidi ni kwamba inasahihisha na kutakasa matendo. Kwa sababu vitendo vyovyote vile, na namna yoyote vitakavyokuwa, haviwezi kuwa sahihi wala kukubaliwa kutoka kwa mtendaji isipokuwa kwa Tauhidi. Kwa maana, Tauhidi kwa matendo ni kama msingi kwa jengo na ni kama mizizi kwa miti. Ndiyo maana akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na anayeitaka Akhera, na akayafanyia juhudi matendo yake, naye ni Muumini, basi hao juhudi yao itakuwa ni ya kushukuriwa." [Surat Al-Isra: 19] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyokuwa wakiyatenda." [Surat An-Nahl: 97] Kwa hivyo, Tauhidi ndiyo inayosahihisha na kuyatakasa matendo. Kwa maana, hata kama mtu ana matendo mengi sana namna gani, hayatakubaliwa kutoka kwake isipokuwa ikiwa yatakuwa yamesimama juu ya Tauhidi. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na hawakuzuiliwa kukubaliwa michango yao ila kwa kuwa walimkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake." [At-Tauba: 54], Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na anayekataa kuamini, bila shaka yameporomoka matendo yake." [Al-Ma’idah: 5], Na alisema: "Na kwa yakini yamefunuliwa kwako na kwa walio kuwa kabla yako: Bila ya shaka ukimshirikisha Mwenyezi Mungu matendo yako yataanguka." [Az-Zumar: 65]; Hivyo basi, Tauhidi husahihisha vitendo, na wala hayawi sahihi bila hiyo.

Vile vile, Tauhidi ndio sababu ya kufaulu na kuinuliwa hapa duniani na akhera. "Hao wapo juu ya uongofu utokao kwa Mola wao Mlezi, na hao ndio waliofaulu." [Surat Al-Baqarah: 5]; Hivyo basi, watu wa Tauhidi ndio watu wa uongofu na watu wa kufaulu, na kufaulu ndilo neno kubwa zaidi linaloweza kusemwa kuhusiana na kupata heri. Aliyefaulu ni yule aliyepata heri ya dunia na akhera, na wala heri haipatikani wala kufikiwa duniani na akhera isipokuwa kwa kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumsafia dini Yeye aliyetakasika na kutukuka:

Na miongoni mwa matunda ya Tauhidi ni kwamba ni sababu ya kupata utukufu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu na Pepo yake, na ni sababu ya kuokoka na adhabu na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo, atakayekutana na Mwenyezi Mungu Mtukufu huku anampwekesha, ataingia Peponi. Na atakayekutana na Mwenyezi Mungu - Mwenyezi Mungu apishe mbali - huku anamshirikisha, ataingia Motoni na atabakia humo milele. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kushirikishwa, na husamehe yaliyo duni ya hilo kwa amtakaye." [An-Nisaa: 48], Hivyo basi, katika athari na matunda ya Tauhidi ni kufaulu kuingia Peponi na kuepuka kutokana na Moto.

Ikiwa mtu ametekeleza Tauhidi kutekeleza kwa faradhi au kule kunakopendekezwa, basi kuokoka kwake ni kuokoka asiingie Motoni. Ama anapokuwa anampwekesha Mwenyezi Mungu lakini alifanya maasi na madhambi yasiyokuwa shirki, basi kuokoka kwake kutakuwa kuokoka kutokana kwa kutokaa humo milele. Kwa sababu hakuna atakayebakia Motoni milele isipokuwa mshirikina, kama ilivyoelezwa katika Hadithi hii: “Atawaamrisha Malaika wamtoe Motoni yeyote ambaye hakuwa akimshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote miongoni mwa wale ambao Mwenyezi Mungu atataka kuwarehemu, miongoni mwa wale wanaosema: " Hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu” ([19]). ( ) Imepokelewa na Bukhari (7437) na Muslim (182) kutoka katika Hadithi ya Abuu Huraira.

Na miongoni mwa matunda yake ni kwamba ndiyo sababu kubwa zaidi ya kukunjuka kwa moyo, na kulingana na namna ya ukamilifu wake, nguvu yake na kuongezeka kwake ndiyo kunakuwa kukunjuka kwa moyo wake.

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Je, yule ambaye Mwenyezi Mungu amemfungulia kifua chake kwa Uislamu, na akawa yuko kwenye nuru itokayo kwa Mola wake Mlezi (ni sawa na mwenye moyo mgumu)?" [Az-Zumar: 22], Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Basi yule ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumuongoa, humfungulia kifua chake kwa Uislamu. Na anayetaka apotee, hukifanya kifua chake kuwa na dhiki, kimebana, kana kwamba anapanda mbinguni." [Al-An’am: 125], Uongofu na Tauhidi ni miongoni mwa sababu kubwa zaidi za kufungua kifua, wakati shirki na upotofu ni miongoni mwa sababu kubwa zaidi za kukifanya kiwe kifinyu.

Na miongoni mwa matunda yake ni kwamba Mwenyezi Mungu aliwahakikishia watu wake heshima na ushindi katika dunia hii, kuwekwa imara katika ardhi na kutengemaa kwa hali zao. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya kuwa makhalifa (watawala) katika ardhi kama alivyowafanya makhalifa wale wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyowapendelea, na atawabadilishia amani baada ya hofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na watakaokufuru baada ya hayo, basi hao ndio wavukao mipaka." [Surat An-Nur: 55].

Na miongoni mwake ni kwamba Tauhidi humfungulia mja mlango wa heri, furaha, raha, shangwe na utulivu. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Wale walioamini na zikatua nyoyo zao kwa kumtaja Mwenyezi Mungu. Hakika kwa kumtaja Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua!" [Surat Ar-Ra'd: 28] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na ukikufikieni uongofu kutoka kwangu, basi atakayeufuata uongofu wangu, hatapotea wala hatataabika. Na atakayejiepusha na utajo wangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu." [Surat Twaha: 123-124].

Na baada ya hayo. Basi hizi ni alama chache kuhusu mada hii kuu, na ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atunufaishe sote kwa yale aliyotufundisha, na ayafanye kuwa ni hoja kwetu na sio dhidi yetu, na atuongoe kwenye njia iliyo sawa.

Na Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye zaidi, na rehema na amani ziwe juu ya mja wake na Mtume wake, Nabii wetu Muhammad, na jamaa zake na Maswahaba wake wote.